MKUU WA MAJESHI JENERALI JACOB JOHN MKUNDA ATEMBELEA MKOA WA RUVUMA KUWAENZI MASHUJAA WA VITA VYA MAJIMAJI
Mkuu wa majeshi Jenerali Jacob John Mkunda katikati mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Kanali Ahmed Abbas akiambatana na viongozi mbalimbali pamoja na Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi CCM Mkoa Oddo Mwisho wakielekea eneo la Mashujaa waliponyongewa

Mkuu wa majeshi Jenerali Jacob John Mkunda akizungumza na wananchi wa Mkoa wa Ruvuma katika Maadhimisho ya Mashujaa wa Vita ya Majimaji Mkoani Ruvuma


Mkuu wa majeshi Jenerali Jacob John Mkunda akikata utepe katika uwanja wa Makumbusho Mkoani Ruvuma wakati wa maadhimisho hayo
Na Regina Ndumbaro -Ruvuma.
Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Tanzania, Jenerali Jacob John Mkunda, ametembelea Mkoa wa Ruvuma kwa lengo la kuwaenzi mashujaa waliopigania uhuru wa nchi katika Vita vya Majimaji.
Ziara hii ni sehemu ya juhudi za serikali za kuenzi historia ya taifa na kuhakikisha kizazi cha sasa kinatambua mchango wa mashujaa wetu katika kupigania uhuru.
Katika hotuba yake, Jenerali Mkunda amesisitiza umuhimu wa maadhimisho haya kwa taifa, akieleza kuwa yanatufundisha thamani ya uzalendo, mshikamano na kujitoa kwa ajili ya nchi yetu.
Ameeleza kuwa historia ya mashujaa wa Vita vya Majimaji ni somo kwa Watanzania wote juu ya umuhimu wa kusimamia haki, uhuru na maendeleo ya taifa letu.
Aidha, Jenerali Mkunda ameongeza kuwa bado kuna changamoto zinazolikabili taifa ambazo ni kuwa ni ujinga, maradhi, umaskini, uvivu, matumizi ya madawa ya kulevya, rushwa na tabia ya kulalamika bila kufanya kazi.
Amesisitiza kuwa kushindwa kupambana na changamoto hizi ni sawa na kusaliti roho za mashujaa waliopigania uhuru.
Pia ameonya dhidi ya mmomonyoko wa maadili unaosababisha kusahaulika kwa tamaduni za taifa.
Ameeleza kuwa kuwaenzi mashujaa wetu siyo tu sehemu ya historia, bali ni ishara ya utambulisho wetu kama taifa.
Akitumia fursa hiyo, Jenerali Mkunda amempongeza Dkt. Nchimbi kwa kuteuliwa kuwa mgombea mwenza wa urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM). Ameeleza kuwa uteuzi wa Dkt. Nchimbi ni heshima kubwa kwa Mkoa wa Ruvuma na unaonyesha imani kubwa aliyonayo ndani ya chama na kwa wananchi wa Tanzania kwa ujumla.
Amehimiza wananchi waendelee kumuunga mkono ili kuhakikisha maendeleo ya nchi yanaendelea kwa kasi na kwa manufaa ya wote.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Kanali Ahmed Abbas Ahmed, ametoa shukrani kwa Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, na Waziri Mkuu Mheshimiwa Kassim Majaliwa kwa jitihada zao za kuenzi historia na mashujaa wa taifa.
Vilevile, amewashukuru viongozi wa dini zote, Baraza la Mila na Desturi, na wadau mbalimbali kwa mchango wao katika kudumisha utamaduni, amani na mshikamano wa kitaifa.
Kanali Ahmed ameendelea kusisitiza umuhimu wa kuhamasisha mila na tamaduni za kale, akibainisha kuwa maadhimisho haya yamekuwa na mchango mkubwa katika kukuza uchumi wa Mkoa wa Ruvuma kutokana na wageni wanaotembelea kutoka maeneo mbalimbali.
Ameeleza kuwa ni jukumu la kila mmoja kuhakikisha kuwa historia na utamaduni wa taifa unadumishwa kwa vizazi vijavyo.
Katika hotuba yake, Jenerali Mkunda pia amewaonya waandishi wa habari dhidi ya kuandika habari zenye lengo la kuwadhalilisha watu.
Katika hitimisho lake, Kanali Ahmed amewataka wananchi wa Ruvuma kujitokeza kwa wingi kushiriki katika Uchaguzi utakaofanyika mwezi Oktoba mwaka huu.
Amesema kuwa ni haki ya kila raia kushiriki katika mchakato wa kidemokrasia na kuhakikisha wanachagua viongozi wanaostahili kwa maendeleo ya taifa.
Pia amewahimiza wananchi kuendelea kuwaombea viongozi wa nchi ili waendelee kuiongoza Tanzania kwa amani, mshikamano na ustawi wa maendeleo.
Maadhimisho haya yameleta mshikamano mkubwa kwa wananchi wa Ruvuma na kuwapa fursa ya kutambua mchango wa mashujaa waliopigania uhuru wa Tanzania.
Tukio hili limewapa wananchi nafasi ya kuenzi historia yao, huku wakihakikisha kuwa uzalendo unaendelea kudumishwa kwa vizazi vijavyo.
from MALUNDE 1 BLOG https://ift.tt/x5DW7Jv
No comments