Breaking News

Msajili wa kampuni azifuta kampuni 11 za LBL

Msajili wa Kampuni kupitia kwa Wakala wa USajili wa Biashara na Leseni (BRELA) ametanaza kuzifuta kampuni 11 za LBL ambazo zimekiuka masarti ya kifungu cha 400A cha Sheria ya Kampuni Sura 212 kwa kufanya shughuli za kibiashara nje ya madhumuni yaliyoainishwa katika Katiba za kampuni hizo na Miongozo ya Uendeshaji wa Kampuni wakati wa usajili.

Akizungumza na waandishi wa habari katika ukumbi wa mikutano uliopo kwenye ofisi za BRELA jijini Dar es Salaam leo tarehe 05 Machi 2025, Afisa Mtendaji Mkuu wa Wakala Bw. Godfrey Nyaisa amebainisha kuwa kampuni hizo zimefutwa kuanzia tarehe 27 Februari 2025 huku sababu kuu ikiwa ni kukiuka Katiba. 

“Sababu za kufuta kampuni hizo ni kukiuka masharti ya Kifungu cha 400A (1) (e) cha Sheria tajwa hapo juu, kwa kufanya shughuli za kibiashara nje ya madhumuni yaliyoainishwa katika Katiba za kampuni hizo na Miongozo ya Uendeshaji wa Kampuni wakati wa usajili.” Alisema Bw. Nyaisa

Bw. Nyaisa alieleza kuwa kifungu hicho cha sheria kikikiukwa, sheria inamtaka Msajili kuchukua hatua chini ya Kifungu hicho 400A (1) (e) ambazo ni kuijulisha kampuni kuhusu ukiukwaji na hatua anazokusudia kuzichukua kwa kampuni husika. 

Aidha, alisema Sheria inaendelea kueleza kuwa, endapo kampuni itashindwa kutoa maelezo, au kutoa maelezo yasiyoridhisha, Msajili atafuta kampuni husika kwenye Rejista ya Kampuni.

“Kwa mujibu wa Kifungu cha 400A (1) (e) Msajili alizijulisha kampuni husika kuhusu kusudio la kuzifuta kupitia notisi zilizotolewa kati ya tarehe 2 na tarehe 26 Januari, 2025, na kwa kuwa kampuni hizo hazikuwasilisha maelezo yoyote kama zilivyotakiwa chini ya kifungu 400A (2), Msajili amezifuta rasmi kampuni hizo” alisisitiza Bw. Nyaisa

Amezitaja Kampuni zilizofutwa kuwa pamoja na LBL Mtwara Media Company Limited (Na. 181289972), LBL Morogoro Media Company Limited (Na. 179770873), LBL Geita Advertising Media Limited (Na. 180439242), LBL Mbeya Media Limited (Na. 179978326), LBL Future Vision Advertising Agency Company Limited (Na. 181302259), LBL Mbezi Advertising Media Company Limited (Na. 180582835), LBL Ubungo Media Limited (Na. 180960333), LBL Mabibo Media Company Limited (Na. 181117346), LBL Mbagala Media Company Limited (Na. 181248874), LBL Gongo la Mboto Media Advertising Company Limited (Na. 181513438), na LBL Dar es Salaam Kigamboni Advertising Company Limited (Na. 180046992).

Katika hatua nyingine msajili ameutaka umma kufahamu kwamba, hakuna sheria wala taasisi yenye mamlaka ya kutoa vibali wala leseni za kufanya biashara za upatu hapa nchini hivyo anaendelea na ufuatiliaji wa kampuni nyingine zinazofanya shughuli za kibiashara nje ya katiba zao na kinyume na Sheria na taratibu, na ataendelea kuzichukulia hatua stahiki ikiwemo kuzifuta kwenye Rejista ya Kampuni.

Vile vile Msajili anaukumbusha Umma kuwa, biashara ya upatu ni kinyume na sheria za nchi na hivyo wananchi wanahimizwa kutoa taarifa mara moja kwa Mamlaka husika, zikiwemo taasisi za Kiserikali na Jeshi la Polisi, ili hatua stahiki zichukuliwe dhidi ya kampuni au watu wanaofanya au kujihusisha na biashara hiyo.


No comments