POLISI YAONYA WANAOSAMBAZA UVUMI WA WIZI WA SEHEMU ZA SIRI ZA WANAUME
Jeshi la Polisi nchini Tanzania limewaonya watumiaji wa Mitandao ya Kijamii wanaosambaza taarifa za uzushi na zisizokuwa na uthibitisho wa Kisayansi kwamba wapo baadhi ya wanaume wanaopoteza sehemu zao za siri mara baada ya kushikwa mabega na baadhi ya watu, uvumi ambao umeripotiwa kwenye Mikoa ya Songwe, Mbeya na Dar Es Salaam na kusababisha vifo vya watu watano na majeruhi kadhaa wanaoendelea kupatiwa matibabu katika maeneo mbalimbali.
Onyo hilo limetolewa katika taarifa iliyosainiwa na Msemaji wa Jeshi la Polisi nchini Tanzania Naibu Kamishna wa Polisi (DCP) David Misime leo Jumamosi Aprili 04, 2026 huku Polisi ikitangaza kuanza kwa uchunguzi na msako mkali kwa walioandaa na kueneza uvumi huo sambamba na kutafuta malengo ya watu hao kueneza taarifa hizo potofu.
"Tabia hizi zinazoongozwa na imani za kishirikina, mihemko ya kishabiki na malengo ambayo hayajabainika hazina ukweli wowote kwani wanaodaiwa kuguswa bega na sehemu zao za siri kutoweka walipokaguliwa sehemu hizo zilikutwa zikiwa maeneo yake kama kawaida na maeneo mengine anayedaiwa kufanywa hivyo alipotafutwa hakuonekana na wala waliokuwa wanashabikia na kuwa wazungumzaji wakuu wakielezea uzushi huo walipotakiwa kumuonesha aliyechukuliwa sehemu zake za siri hawakuweza kumuonesha wala kutoa uthibitisho." Amesema Kamanda Misime.
Kulingana na Polisi, Uvumi huo ulianza kuibuka katika maeneo ya Tunduma Mkoani Songwe Aprili Mosi, 2026 na kusababisha vifo vya watu watano na wengine wawili kujeruhiwa na baadae matukio kama hayo kuripotiwa Makongolosi Jijini Mbeya na watu wawili kujeruhiwa kabla ya jana Aprili 03, 2026 kuripotiwa katika eneo la Kimara Mwisho na Mbezi Shule Jijini Dar Es Salaam na leo Jumamosi kujitokeza tena matukio mawili Mkoani Mbeya na kusababisha kujeruhiwa kwa watu wawili na uchunguzi wa Madaktari ulipofanyika kwa wanaodai kushikwa bega ilithibitika kuwa hawakuwa na mabadiliko yoyote.
from MALUNDE 1 BLOG https://ift.tt/rMaiP61

No comments