MOI YAENDELEA KUNG’ARA KATIKA MATIBABU YA MIFUPA BARANI AFRIKA.
Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI) imeemdelea kung’ara katika matibabu ya kibingwa na kibobezi za mifupa barani Afrika baada ya kuendelea kuandaa mafunzo ya 10 kuhusu mbinu mpya na za kisasa za matibabu ya majeraha na mifupa kwa wataalam barani Afrika kwa kushirikiana na Taasisi ya Kimataifa ya Tiba ya Mifupa na Majeraha (IGTO) ya nchini Marekani.
Mafunzo hayo yamefunguliwa leo Jumanne Mei 27, 2025 katika ukumbi wa CHPE, uliopo Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) ambapo Mkurugenzi Mtendaji wa MOI, Mhe. Balozi Dkt. Mpoki Ulisubisya ambaye amesema kuwa ushirikiano kati ya MOI na Taasisi za Kimataifa umekuwa chachu katika kuwajengea uwezo madaktari wazawa na kuwapa mbinu mpya na za kisasa za matibabu y majeraha na mivunjiko ya mifupa.
"Kwa mara ya 10 mkutano huu unaleta pamoja wataalamu kutoka nchi mbalimbali katika bara la Afrika, kwa ajili ya kujifunza mbinu mpya na za kibobezi za kutibu magonjwa mbalimbali ya mifupa" amesema Dkt. Mpoki na kuongezea
"Umoja huu umefanikisha matibabu yetu kuwa ya hali ya juu sana... Mivunjiko ya mifupa mingi ambayo zamani ilikuwa ngumu kuiunga lakini kwa sasa inatibika kwa urahisi".
Aidha, Mwenyekiti mwenza wa IGTO, Prof. David Shearer kutoka Marekani ambaye pia ni mmoja wa wakufunzi wa mafunzo hayo, amesema kuwa ana furaha kuwa nchini Tanzania na kushuhudia maendeleo makubwa yaliyofikiwa na MOI katika sekta ya mifupa.
"Ni furaha kubwa kuwa hapa Tanzania kwa mara nyingine tena, tumekuwa tukishirikiana na MOI kwa miaka kadhaa sasa na tunavutiwa sana na juhudi kubwa wanazofanya katika kutoa huduma bora na kuwa tayari kujifunza" amesema Prof. David
Naye, Mratibu wa mafunzo hayo, kutoka MOI, Dkt.William Mgisha ambaye pia ni daktari bingwa wa mifupa, amesema kuwa mafunzo hayo ni ya awamu ya 10 tangu kuanzishwa kwa ushirikiano baina ya taasisi hizo mbili.
Kwa upande wake, mshiriki wa mafunzo hayo kutoka MOI, Dkt. Zakayo Wangwe, amesema mafunzo ni muhimu kwa sababu yanawaongezea ujuzi wa kitaalamu ambao unawasaidia kuboresha huduma wanazozitoa kwa wagonjwa katika maeneo yao ya kazi.
No comments