Breaking News

HERITAGE CAMP & LODGE YATOA AJIRA 100, YAPANUA MBAWA KUTANGAZA UTALII KIMATAIFA

 

Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Heritage Camp & Lodge, Erick Mashauri akiongea na waandishi wa habari 

Na Woinde Shizza Arusha

Wamiliki wa kampuni za utalii nchini wameiomba serikali kuwasaidia katika kugharamia ushiriki wao kwenye maonyesho ya utalii ya kimataifa, ili kuwawezesha kutangaza vivutio vya utalii vya Tanzania na kukuza soko la sekta hiyo muhimu kiuchumi.

Wakizungumza katika maonyesho ya utalii ya KARIBU KILI FAIR yaliyofanyika jijini Arusha, baadhi ya wamiliki wa kampuni hizo walisema kuwa licha ya dhamira yao ya kutangaza nchi, changamoto ya gharama za usafiri na malazi imekuwa kikwazo kikubwa, hasa kwa kampuni ndogo na zinazochipukia.

Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Heritage Camp & Lodge, Erick Mashauri, alisema kuwa ni wakati muafaka kwa serikali kuingilia kati kwa kusaidia gharama kwa kampuni zinazotaka kushiriki kwenye maonyesho ya kimataifa, jambo ambalo litasaidia sio tu kukuza biashara zao bali pia kuitangaza Tanzania kwa ujumla wake.

"Kinachohitajika ni msaada wa serikali ili watu waweze kushiriki kwenye maonyesho, hususan kampuni changa ,Kwa mfano, tunapokuwa na maonyesho ya utalii Ujerumani, ndege zetu kama Air Tanzania ziweze kusaidia kuwasafirisha wajasiriamali wa utalii kwa gharama nafuu, kama inavyofanyika kwa wanamichezo na mashabiki," alisema Mashauri.

Aliongeza kuwa serikali inaweza pia kusaidia kwa kutoa nusu ya gharama za usafiri  hatua ambayo itawapa wamiliki wa kampuni fursa ya kushiriki katika maonyesho makubwa duniani na hivyo kuongeza watalii wanaoitembelea Tanzania.

Kwa upande mwingine, Mashauri alieleza kuwa kampuni yake ya Heritage Camp & Lodge imeajiri wafanyakazi zaidi ya 100, na ina mpango wa kuongeza ajira zaidi ya 150 kupitia mradi mpya wa hoteli ya nyota tano iitwayo Hakuna Matata Safari Lodge inayojengwa katika eneo la Serengeti.

"Mradi huu utakapokamilika si tu utaongeza ajira kwa Watanzania, bali pia utaongeza mapato ya serikali kupitia kodi na tozo mbalimbali," alibainisha.

Katika juhudi za kuhamasisha utalii wa ndani, Mashauri alisema kampuni yake inatoa punguzo la asilimia 30 kwa watalii wazawa kulingana na msimu, ili kuwavutia zaidi Watanzania kutembelea vivutio vyao.

Aidha, aliwahimiza Watanzania kufika katika camp na lodge zao ambapo huduma bora zinapatikana, ikiwemo chakula kitolewacho bila mipaka kwa wateja waliolipia, huduma za vinywaji kama maji, maziwa na kahawa bila malipo, pamoja na mapishi bora yanayowafurahisha wateja wote.

"Huduma zetu ni za kiwango cha juu na tunatoa thamani halisi kwa pesa ya mteja Tunawaalika Watanzania waje wajionee wenyewe tofauti yetu," alisisitiza Mashauri.



from MALUNDE 1 BLOG https://ift.tt/n32CUza

No comments