Rais Samia apokea Sh1 trilioni kama gawio na michango mingine.
Dar es Salaam.
Rais wa Tanzania Mhe. Dk. Samia Suluhu Hassan Leo, Juni 10, 2025 amepokea kiasi cha Sh1.028 trilioni kama gawio na michango kutoka mashirika ya umma yaliyo chini ya usimamimizi wa Ofisi ya Msajili wa Hazina (OMH) na Kampuni ambazo Serikali ina hisa chache.
Makusanyo hayo ya kihistoria tangu kuanzishwa kwa Ofisi ya Msajili wa Hazina mwaka 1959, ni ongezeko la asilimia 68 ya kiasi kilichokabidhiwa mwaka jana kipindi kama hiki na asilimia 34 ya makusanyo yote ya mwaka 2023/24, ambayo yalikuwa ni Sh767 bilioni.
Kuna uwezekano wa takwimu hizo kupaa zaidi kwani makusanyo bado yanaendelea mpaka Juni 30 mwaka huu, ongezeko linaloshuhudiwa ni matokeo ya mwitikio chanya wa taasisi za umma katika kutekeleza maelekezo ya Mhe. Rais ya kuongeza tija na ufanisi.
Ni katika muktadha huo, Rais Samia alionesha kuridhishwa na mwenendo huu ambao ni matokeo ya utekelezaji wa maelekezo yake kwa taasisi kuongeza tija na ufanisi katika utendaji.
Alieleza kuwa anajivunia uwekezaji wa Sh86.3 trilioni uliofanywa na serikali kwenye taasisi za umma na kampuni zinazomilikiwa kwa sehemu na Serikali.
Pamoja na mafanikio hayo, Rais Samia alisema kiwango hiki bado hakijafikia matarajio ya Serikali juu ya mchango wa Mashirika na Taasisi za Umma katika mfuko mkuu wa Serikali wa mapato yasiyo ya kikodi kutoka kwa Taasisi za Umma.
“Lengo letu ni kufikia angalau Shilingi trilioni 1.5 kwa mwaka ujao, na nina imani tunaweza,” alisema.
Aliongeza: “Nikutake, Msajili wa Hazina (Nehemiah Mchechu), kuzipitia taasisi zote na kuweka malengo mahsusi ya mapato kwa kila moja, ili tuweze kufikia azma hiyo.
Ili kuongeza ufanisi katika utendaji wa mashirika na hatimaye ukusanyaji mapato yasiyo ya kikodi na utoaji gawio mwakani, Mhe. Rais aliagiza mambo manne.
Kwanza, Taasisi kuwa wabunifu kwa lengo la kuongeza ufanisi katika utendaji na kutatua changamoto zinazowakabili.
“Mageuzi ni pamoja na kuwa wabunifu, tusisubiri Serikali itatue kila changamoto inayotukabili kama taasisi. Tutumie fursa mbalimbali zinazotuzunguka katika kutatua changamoto hizo ikiwemo soko la mitaji,” alisema Mhe. Rais.
Sanjari na hilo, Mhe. Rais alimwagiza Waziri wa Mipango na Uwekezaji Mhe. Kitila Mkumbo kuendelee kusimamia ukamilishaji wa Sheria ya Uwekezaji wa Umma.
“Ili kuwezesha usimamizi madhubuti wa uwekezaji wa Serikali, tunapaswa kuhakikisha kuwa tunakuwa na Sheria ya Uwekezaji wa Umma ikiwemo suala la Mfuko,” alisisitiza.
Sambamba na hilo, Mhe. Rais alimuagiza Msajili wa Hazina pamoja na vingozi wote wa Taasisi za Umma kuendelea kubuni na kusanifu mifumo ya TEHAMA.
Alisema mifumo ya TEHAMA mahsusi itaongeza ufanisi na tija katika utekelezaji wa majukumu yao na hatimae kusaidia utoaji huduma wa haraka na kuongeza faida kutokana na uwekezaji uliopo.
“Ninataka muendelee kuhuisha mifumo ya TEHAMA iliyopo ili iweze kuwa na mlingano mzuri wa taarifa na kuongeza tija kwa taasisi zetu,” alisisitiza.
Mwisho, Mhe. Rais aliiagiza Ofisi ya Msajili wa Hazina na Mamlaka nyingine husika kuendelea na jitihada za jumla za kuwajengea watumishi uwezo katika nyanja mbalimbali za kisasa pamoja na motisha stahiki.
“Kwa kufanya hivi kutasaidia kuongeza morali ya kazi na hatimae tija kwa taasisi zetu,” alisema.
Akizungumza awali, Msajili wa Hazina Bw. Mchechu alisema kiasi cha Sh1.028 trilioni kimekusanywa kutoka katika jumla ya taasisi na Mashirika 213 (195 ya umma na 18 Kampuni zenye hisa chache).
Hii inamaanisha kuwa Mashirika 57 hayajatoa gawio bado--- ambayo ni asilimia 22 ya Mashirika yote.
“Tutaendelea kuimarisha usimamizi ili kuhakikisha mashirika ya umma yanaendelea kuchangia ipasavyo katika maendeleo ya kiuchumi na kijamii,” alisema Bw. Mchechu.
Kati ya Sh1.028 trilioni zilizokusanywa mwaka huu wa fedha, gawio kutoka Mashirika na Kampuni zinazofanya biashara ni asilimia 59 ya makusanyo yote.
Aidha, michango ya asilimia 15 ya mapato ghafi imechangia asilimia 35, huku mapato mengineyo yanayojumuisha ziada, marejesho ya mikopo na riba pamoja na Mawasilisho yatokanayo na mtambo wa kuhakiki na kuwezesha mawasiliano (TTMS) yakichangia asilimia sita ya mapato yote.
“Takwimu hizi ni ushahidi wa mwelekeo chanya na matokeo ya juhudi za mageuzi ya kiuendeshaji tunayotekeleza kwa maelekezo yako, Mheshimiwa Rais,” alisema Bw. Mchechu.
Alisema pamoja na mafanikio yote bado kuna kazi kubwa ya kuendelea kufanya, linapokuja suala la maboresho ya kiutendaji na kiuendeshaji.
Bw. Mchechu alisema miongoni mwa kazi zilizopo mbele ni kuhakikisha idadi ya mashirika yanayochangia katika Mfuko Mkuu wa Serikali inaongezeka.
Pia, alisema inatakiwa kupunguza utegemezi wa ruzuku ya Serikali katika uendeshaj na Mashirika yanayojiendesha kwa hasara yanaondoka katika kundi hilo.
“ Mashirika yameendelea kutekeleza kwa kiu na msukumo mkubwa falsafa yako ya R4 ambapo ofisi yangu pamoja na Mashirika tumejikita katika R2 yaani Reforms and Rebuild,” alihitimisha Bw. Mchechu.
Kwa upande wake Mhe. Waziri Prof. Kitila aliahidi kuendelea kuhakisha wizara yake inasimamia kikamilifu maono ya Mhe. Rais ya kuhakikisha mashirika ya umma yanaendelea kutoa matokeo bora kwa maendeleo ya Taifa.
Katika mwaka ujao wa fedha 2025/26, Wizara kupitia Ofisi ya Msajili wa Hazina imejipanga kutekeleza mikakati thabiti ya kuimarisha usimamizi na tathmini ya utendaji wa taasisi na mashirika ya umma
“Lengo letu ni kuongeza ufanisi na kuhakikisha taasisi hizi zinaendelea kutoa matokeo bora zaidi kwa manufaa ya Watanzania,” alisema Prof. Kitila.
Katika tukio hilo la kihistoria ‘ Gawio Day’, Rais Samia alitoa tuzo kwa taasisi 14 zilizofanya vizuri zaidi kwa mwaka wa fedha 2024/2025.
Washindi walichaguliwa kwa kuzingatia vigezo vya mchango mkubwa kwa Serikali, uendelevu wa michango, ukuaji wa michango, na mageuzi ya kiutendaji.
Katika kundi la taasisi zilizotoa gawio kubwa zaidi, Twiga Minerals Corporation iliongoza kwa kutoa Sh93.6 bilion, ikifuatiwa na Airtel Tanzania kwa Sh73.9 bilioni, na NMB Bank Plc kwa Sh68.2 bilioni.
Ushindi wao umeonesha mchango mkubwa wa sekta binafsi na ubia katika mapato ya serikali.
Katika kundi la taasisi zinazochangia asilimia 15 ya mapato ghafi, Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari (TPA) iliongoza kwa Sh181.1 bilioni, ikifuatiwa na Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA)----Sh38.8 bilioni na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS)----Sh29.8 bilioni.
TPA inaendelea kuwa nguzo muhimu ya mapato kutokana na nafasi yake katika biashara na usafirishaji.
Kwa taasisi zilizoongeza michango yao kwa kasi zaidi, Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) na Benki ya Kilimo Tanzania (TADB) ziliongoza.
TPDC iliongeza gawio lake kwa asilimia 100, NHC kwa asilimia 363 na Benki ya Kilimo kwa asilimia 285.
Hii ni dalili ya mwelekeo mzuri wa mageuzi na uwekezaji unaozaa matunda.
Katika kundi la taasisi zilizotoa mchango mfululizo kwa miaka mitano, Mamlaka ya Mawasiliano (TCRA), Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) na Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) zilitambuliwa kwa uendelevu na nidhamu ya kifedha.
Uwezo wao wa kuchangia kila mwaka kwa kiasi kikubwa unaonesha uthabiti wa kiuendeshaji.
Tuzo maalum ilitolewa kwa TAZAMA, taasisi iliyotoka kwenye hasara ya muda mrefu na kuanza kutoa faida endelevu, huku ikiongeza gawio lake kwa asilimia 1,214 katika kipindi cha miaka mitano.
Hili ni somo kwa mashirika mengine kuwa mageuzi yanawezekana kwa nia, mbinu sahihi na uongozi makini.
Benki Kuu ya Tanzania (BoT) ilipewa tuzo ya mchango wa kipekee na wa aina yake katika Mfuko Mkuu wa Serikali.
No comments