LIGI YA DUMISHA AMANI YAANZA KUTIMUA VUMBI SHINYANGA
Na Marco Maduhu,SHINYANGA
LIGI ya dumisha Amani imeanza kutimua vumbi katika Kata 14 za Halmashauri ya wilaya ya Shinyanga.
Ligi hiyo imezinduliwa leo Juni 8,2025 katika Kata ya Tinde.
Mdhamini wa ligi hiyo Fadhili Nafutari, ambaye ni mdau wa michezo,amesema lengo lake ni kuhamasisha amani, kuibua na kukuza vipaji vya vijana kupitia mpira wa miguu.
Amesema michezo ni sehemu ya kufikisha ujumbe kwa jamii,juu ya kuendelea kudumisha amani ya nchi, pamoja na kuibua na kukuza vipaji vya vijana, na hata kupata ajira kwa kusajiliwa na timu kubwa.
“Mpira ni maendeleo,Ajira na hujenga undugu, sababu ya kukutanisha watu kutoka maeneo mbalimbali na kudumisha amani,hivyo nawasihi vijana watumie pia fursa ya Ligi hii kuonyesha vipaji vyao,”amesema Nafutari.
Naye Mkaguzi Msaidizi wa Jeshi la Polisi ambaye ni Polisi Jamii Kata ya Tinde Beda Lutego,amewasisitiza wananchi kwamba, waitumie michezo hiyo katika kuendelea kudumisha amani ya nchi,pamoja na kuwafichua wahalifu.
Awali Mratibu wa Ligi hiyo Sungi Leonard,amesema Timu 32 zitashiriki kucheza kutoka Kata 14 za Halmashauri ya wilaya ya Shinyanga,ambazo zitacheza kuanzia hatua ya makundi hadi kufikia fainali, na itakwenda hadi Julai 6 mwaka huu.
Nao baadhi ya vijana akiwamo Alex Holy, wamesema ligi hiyo ni fursa kwao katika kuonyesha vipaji vyao,huku akitoa wito kwa wadau wa michezo, kwamba wafike kuona vipaji vya vijana na hata kuwatafutia usajili kwenye Timu kubwa na kupata Ajira.
Aidha,wakati wa uzinduzi wa ligi hiyo,ilitanguliwa pia na michezo mingine zikiwamo Mbio za Baiskeli kwa wanawake na wanaume,ngoma za jadi kwa kucheza na nyoka,pamoja na utangulizi wa mechi kati ya Mizani na Young Star ambapo walitoka suluhu ya goli moja kwa moja.
TAZAMA PICHA👇👇
Mdhamini wa ligi ya dumisha Amani Fadhili Nafutari akizungumza.
Mkaguzi Msaidizi wa Jeshi la Polisi ambaye ni Polisi Jamii Kata ya Tinde Beda Lutego akizungumza.
Diwani wa Tinde Jafari Kanolo akizungumza.
Mratibu wa Ligi ya dumisha Amani Sungi Leonard,akizungumza.
Mdhamini wa ligi ya dumisha Amani Fadhili Nafutari,akipiga penat kuzindua mashindano hayo.
Mdhamini wa Ligi ya Dumisha Amani Fadhiri Nafutari akikabidhi Jezi na Mpira kwa Timu 32 ambazo zinashiriki Ligi hiyo.
from MALUNDE 1 BLOG https://ift.tt/CV6bUxQ
No comments