Breaking News

MILA POTOFU ZINAVYO CHOCHEA MIMBA ZA UTOTONI NA KUATHIRI NDOTO ZA VIJANA WILAYANI CHEMBA


Mwezeshaji wa mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP) Vena Assenga (kulia) akizungumza na makundi mbalimbali wakiwemo wazee wa mila,viongozi wa dini,na watendaji wa serikali kwenye mdahalo uliowakutanisha kwa ajili ya kujadili usawa wa kijinsia na kuondoa vikwazo kwa wanawake na vijana  wilaya ya Chemba . 

Na Dotto Kwilasa, DODOMA

Katika kijiji cha Kidoka, wilayani Chemba, mkoa wa Dodoma, mdahalo wa wazi umeibua mjadala mzito kuhusu athari za mila na desturi potofu zinazofanyika katika jamii kwa kisingizio cha kuenzi utamaduni wa Mtanzania.

Mdahalo huo ulioandaliwa kwa ufadhili wa Ubalozi wa Ireland kupitia mradi wa Tuinuke kwa Pamoja, umebaini kuwa mila zinazohusishwa na ngoma za unyago na jando zimegeuka chanzo kikuu cha mimba za utotoni, utoro mashuleni, na kuvunjika kwa ndoto za vijana wengi.

Wazee wa kimila, viongozi wa dini, akina mama, wawakilishi wa serikali za vijiji na mashirika ya kiraia walishiriki mdahalo huo uliolenga kutafuta njia za kufanikisha usawa wa kijinsia na kuondoa vikwazo vinavyowakwamisha wanawake na vijana.

Sheikh Salamu Hando, mmoja wa washiriki kutoka Kidoka, ameeleza kwa uchungu jinsi baadhi ya ngoma za unyago zinavyohusisha mafundisho yenye mwelekeo wa ngono kwa watoto wa kike ambao bado hawajafikia umri wa utu uzima.

“Tunawaambia watoto kuwa sasa wamekuwa watu wazima, huku tukiwafundisha stadi za ndoa na tendo la ndoa, jambo ambalo linawapotosha na kuwasukuma kwenye majaribu ya mapenzi kabla ya wakati,” amesema Sheikh Hando.

Naye Arafa Hukomo, mjumbe wa kituo cha taarifa na maarifa katika kijiji hicho, ameongeza kuwa kutokana na kukosekana kwa sheria kali za kudhibiti desturi hizo, baadhi ya wasichana huishia kupata ujauzito wakiwa bado wadogo.

"Matokeo yake ni watoto wa kike kuacha shule na kukosa fursa ya kujitegemea baadaye kimaisha," ameeleza Hukomo.

Mbali na wasichana, vijana wa kiume nao wameathirika,Wengi wao hutoroka shule na kukimbilia mijini wakisaka ajira zisizo rasmi ili kujitafutia kipato, hatua ambayo huwapeleka mbali na ndoto zao za kielimu.

Amesema, “Jamii inawafanya vijana waamini kuwa mtu mzima ni yule anayeweza kujitegemea kiuchumi, hata kwa njia isiyo rasmi,” alisema mmoja wa washiriki wa mdahalo.

Kwa upande wake Afisa Maendeleo ya Jamii wa kijiji hicho, Samalu Lupande, ameangazia kiini kingine cha tatizo kuwa ni umaskini wa kaya.

Amesema kuwa wazazi wengi, hasa katika familia masikini, huwalazimisha au kuwasihi watoto wao wasome kwa kiwango cha kawaida tu, au hata kuacha shule, ili wawasaidie katika shughuli za kiuchumi.

Amesena wazazi wengine huwashawishi watoto wasifanye vizuri kwenye mitihani ili wasiendelee na masomo,hii hutokea kwa sababu hawana uwezo wa kugharamia elimu ya juu,” amesema.

Mbali na hayo,ameeleza kuwa umasikini umekuwa kichocheo cha wasichana kujiingiza kwenye mahusiano ya kingono kwa ajili ya kujikimu.

“Mtoto anakwenda shuleni bila chakula, hana vitabu, hana sare za shule anapotokea mtu kumsaidia, hata kama kwa masharti ya rushwa ya ngono, anakubali,hii ni hatari kwa maendeleo ya jamii,” anafafanua Lupande.

Kutokana na hayo Mwezeshaji kutoka Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP) Vena Assenga amesisitiza kuwa lengo kuu la mdahalo huo ni kuchochea mabadiliko ya kijamii kupitia utungaji wa sheria rafiki kwa mtoto wa kike.

Ameeleza kuwa si mila zote ni mbaya, lakini ni muhimu kuchuja yale maudhui ambayo yanapingana na ustawi wa watoto na vijana.

“Tunapaswa kutofautisha kati ya ngoma kama sanaa ya utamaduni na mafundisho yake.

Tukiweka sheria madhubuti, tutaweza kubaki na utamaduni wetu bila kuharibu maisha ya watoto wetu,” amesema Assenga.

Naye Deogratius Temba, mwezeshaji wa mradi wa Tuinuke kwa Pamoja unaotekelezwa Chemba na Kondoa kwa ufadhili wa Ubalozi wa Ireland, ameeleza kuwa mradi huo umejikita katika kuondoa vikwazo vya kijinsia vinavyomkandamiza mwanamke na kijana.

Ameeleza kuwa kupitia mijadala na midahalo ya kijamii kama hii, jamii huamshwa kiakili na kijamii, na hivyo kuwa tayari kubadilika.

Mjadala huu unaashiria mwamko mpya katika wilaya ya Chemba,mwamko wa kuhoji na kuchuja maudhui ya mila na desturi zetu.

Amesema ni dhahiri kuwa jamii inahitaji mabadiliko ya haraka kwa mila zisizofaa ili kuwaepusha watoto wa kike na wa kiume dhidi ya athari zinazotokana na desturi potofu.

"Tunafahamu tunawajibu wa kuzitii mila na tamaduni zetu, lakini jamii yetu inafaa kufahamu kuwa kuna mila hazifai kuzingatiwa kwa kuwa zimepitwa na wakati, ni wajibu wa kila mdau kushiriki katika mapambano haya kwa kuweka mbele maslahi ya watoto na kizazi kijacho, amesisitiza.

Pamoja na mambo mengine Mdahalo huo ulioandaliwa kwa ufadhili wa Ubalozi wa Ireland kupitia mradi wa Tuinuke kwa Pamoja, ulibaini kuwa mila zinazohusishwa na ngoma za unyago na jando zimegeuka chanzo kikuu cha mimba za utotoni, utoro mashuleni, na kuvunjika kwa ndoto za vijana wengi.




from MALUNDE 1 BLOG https://ift.tt/zeMf8Oi

No comments