Breaking News

OFA YA RAIS SAMIA YAREJESHA HUDUMA YA MAJI KWA MAMIA YA WAKAZI WA SONGEA

Mkurugenzi wa Mamlaka ya huduma  safi na usafi wa mazingira kwa wateja wa Songea (SOUWASA), Bi. Baby Lucas Bicco akizungumzia kuhusu umuhimu wa Ofa iliyotolewa na Mheshimiwa Rais kwa wateja waliositishiwa huduma hiyo ya maji safi na usafi Songea Mkoani Ruvuma


Na Regina Ndumbaro Songea-Ruvuma 

Ofa iliyotolewa na Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan ya kurejesha huduma ya maji bure kwa wateja waliokatiwa huduma hiyo kutokana na madeni, imewanufaisha wakazi 287 wa Manispaa ya Songea, Mkoa wa Ruvuma. 

Mkurugenzi wa Huduma kwa Wateja wa Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Songea (SOUWASA), Bi. Baby Lucas Bicco, amesema kuwa utekelezaji wa agizo hilo la Rais umefanyika kwa mafanikio makubwa kupitia kampeni mbalimbali za kuwafikia wateja waliositishiwa huduma.

Bi. Bicco amesema kuwa SOUWASA ilitumia njia mbalimbali kuwafikia wateja hao, ikiwemo kuwatafuta kwa njia ya simu, matangazo ya magari mitaani na ujumbe wa moja kwa moja kwa kila mteja. 

Kupitia juhudi hizo, hadi kufikia Mei 31, 2025, jumla ya wateja 287 walikuwa wameunganishiwa tena huduma ya maji bila gharama yoyote, na makubaliano maalum ya kulipa madeni yao polepole yalifikiwa.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, kabla ya kuanza kwa ofa ya Rais iliyodumu kuanzia Mei 8 hadi 31, 2025, jumla ya wateja 2,400 walikuwa wamesitishiwa huduma kutokana na sababu mbalimbali, zikiwemo malimbikizo ya ankara. 

Katika kipindi hicho cha ofa, zaidi ya shilingi milioni 15 zilikusanywa kutoka kwa wateja waliokuwa na deni la jumla ya zaidi ya milioni 22, jambo linaloashiria mafanikio makubwa katika ukusanyaji wa mapato.

Aidha, Bi. Bicco ametoa wito kwa wateja wote wa maji kuhakikisha wanalipa ankara zao kwa wakati ili kuepuka usumbufu wa kusitishiwa huduma, kwani kuchelewesha malipo hupelekea kuongezeka kwa madeni na gharama za kurejesha huduma. 

Ameeleza kuwa mteja anayelipa kwa wakati anapata siku 30 za kulipa kwa hiyari bila adhabu yoyote, jambo linalomuepusha na changamoto za kifedha zinazoweza kutokea baadaye.

Kwa upande mwingine, Mamlaka hiyo imesisitiza kuwa kwa wateja ambao hawakufanikiwa kunufaika na ofa hiyo, bado wana nafasi ya kufika katika ofisi za SOUWASA na kuzungumza kuhusu namna ya kurejeshewa huduma.

 Amesema changamoto za kifedha ni tofauti kwa kila mteja, hivyo mamlaka iko tayari kusikiliza na kusaidia kwa kutoa fursa ya makubaliano maalum ya kulipa madeni hatua kwa hatua bila shuruti, ili kila mwananchi aweze kupata haki yake ya msingi ya huduma ya maji safi na salama.



from MALUNDE 1 BLOG https://ift.tt/hOYTZdR

No comments