Breaking News

GCLA yajivunia kuongeza kasi ya uchunguzi wa kisayansi nchini






-Yasema uwekezaji wa serikali waongeza ufanisi wa uchunguzi wa vinasaba na kemikali
-Sayansi jinai yaipaisha GCLA mafanikio makubwa chini ya Serikali ya Awamu ya Sita

Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali (GCLA) imefanikiwa kuongeza kasi na ubora wa utoaji wa matokeo ya uchunguzi wa sayansi ya jinai, huduma za vinasaba, usimamizi wa kemikali na uthibiti wa ubora wa bidhaa kwa kiwango kikubwa, kufuatia uwekezaji mkubwa wa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Akizungumza jijini Dar es Salaam tarehe 10 Julai 2025 wakati wa kikao kazi na wahariri na waandishi wa habari kilichoandaliwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina, Mkemia Mkuu wa Serikali Dkt. Fidelice Mafumiko alisema kuwa mafanikio haya yametokana na usasa wa vifaa na teknolojia iliyowekezwa katika maabara, hasa katika kitengo cha vinasaba.

Kwa mujibu wa Dkt. Mafumiko, thamani ya mitambo iliyopo katika mamlaka hiyo imeongezeka kutoka shilingi bilioni 13.6 mwaka 2017/2018 hadi shilingi bilioni 17.8 mwaka 2024/2025 – ongezeko la asilimia 23.6. Fedha hizo zilitumika kununua mitambo mikubwa 16 na mingine midogo 274, hatua iliyoboresha kwa kiasi kikubwa ufanisi wa uchunguzi wa kimaabara kwa wananchi kote nchini.

Aidha, mamlaka hiyo imefanikiwa kuongeza idadi ya wadau waliosajiliwa kutoka 2,125 mwaka 2021 hadi 3,835 kufikia Juni 2025 – ongezeko la asilimia 81, sambamba na kukagua jumla ya maghala 8,521 ya kuhifadhia kemikali, ikilinganishwa na lengo la 7,160, sawa na utekelezaji wa asilimia 119.

Katika eneo la udhibiti wa kemikali, vibali vya kuingiza kemikali nchini vimeongezeka kutoka 40,270 mwaka wa fedha 2020/2021 hadi 67,200 mwaka wa fedha 2024/2025 – ongezeko la asilimia 40. Hali hiyo imechochea mazingira mazuri ya biashara hususan katika sekta ya madini.

Matumizi ya kemikali muhimu pia yameongezeka kwa kasi kubwa katika kipindi cha miaka minne iliyopita. Kwa mfano, kiasi cha Ammonium Nitrate kilichotumika kimepanda kutoka tani 135,445 mwaka 2021/2022 hadi tani 461,777.42 mwaka 2025 – ongezeko la asilimia 241. Vilevile, matumizi ya Salfa yamefikia tani 1,867,104.72 kutoka tani 396,982 (ongezeko la asilimia 370.32) huku Sodium Cyanide ikiongezeka kwa asilimia 52.20 hadi tani 63,103.4.

Dkt. Mafumiko alieleza kuwa asilimia 80 ya Ammonium Nitrate yote huingia nchini kupitia Bandari ya Tanga, ishara ya mafanikio ya uwekezaji wa serikali katika miundombinu ya bandari hiyo.

Kwa upande wake, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano wa Ofisi ya Msajili wa Hazina, Bw. Sabato Kossuri, alisema kuwa vikao vya aina hiyo vina lengo la kuimarisha ushirikiano kati ya vyombo vya habari na taasisi za serikali, ili kuwezesha utoaji wa taarifa sahihi na uelewa mpana kwa umma kuhusu huduma na mafanikio ya taasisi hizo.

GCLA, ambayo ilianzishwa kwa mujibu wa Sheria Na.8 ya Mwaka 2016, imepitia hatua mbalimbali za kimabadiliko kutoka idara ya wizara, hadi kuwa wakala (1999–2016) na sasa kuwa mamlaka kamili tangu Aprili 5, 2017. Asili yake inaanzia mwaka 1895 kama kituo cha utafiti wa magonjwa ya ukanda wa joto kabla ya kuhamia Wizara ya Afya mwaka 1947 baada ya Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia.

No comments