KATIBU TAWALA WILAYA YA KAHAMA AWAPONGEZA WASHIRIKI WA MAONESHO YA SABASABA 2025 KUTOKA MKOA WA SHINYANGA

Katibu Tawala wa Wilaya ya Kahama, Bi. Glory Absalum, amewapongeza wafanyabiashara kutoka Mkoa wa Shinyanga wanaoshiriki Maonesho ya 49 ya Biashara ya Kimataifa ya Sabasaba, yanayoendelea katika Viwanja vya J.K Nyerere, jijini Dar es Salaam.
Akizungumza mara baada ya kutembelea mabanda ya washiriki hao yaliyopo ndani ya Banda la Sadan, mkabala na Banda la TANESCO, Bi. Glory amepongeza ubunifu mkubwa unaofanywa na wafanyabiashara hao, hususan katika kuongeza thamani ya bidhaa mbalimbali walizonazo.
“Nawapongeza kwa dhati wafanyabiashara wote kutoka Halmashauri zote za Mkoa kwa ushiriki wenu mzuri. Maonesho haya ni fursa adhimu ya kuuza bidhaa zenu, kutangaza huduma mnazotoa pamoja na kuonesha fursa zilizopo katika maeneo yenu. Huu ni wakati muafaka wa kushirikiana na wafanyabiashara wa ndani na nje ya nchi,” alisema Bi. Glory.
Aidha, ameeleza kuwa kiwango cha maandalizi na ubora wa bidhaa zinazotolewa na washiriki kutoka Mkoa wa Shinyanga ni ushahidi wa uwezo mkubwa walionao na utayari wa kushindana katika masoko ya Kitaifa na Kimataifa.
Mabanda ya Mkoa wa Shinyanga yamekuwa kivutio kikubwa kwa wageni mbalimbali wakiwemo viongozi wa Serikali, wafanyabiashara wa ndani na nje ya nchi pamoja na wananchi, kutokana na ubunifu, nidhamu ya kazi na bidhaa zenye viwango vya juu vinavyoendana na mahitaji ya soko.
Maonesho ya Biashara ya Kimataifa ya Sabasaba ni jukwaa muhimu kwa wafanyabiashara na taasisi mbalimbali kuonesha bidhaa, huduma na teknolojia mpya, huku yakihamasisha uwekezaji ndani ya Mkoa wa Shinyanga na ushirikiano wa kibiashara kati ya Tanzania na mataifa mengine.
from MALUNDE 1 BLOG https://ift.tt/z2o6Htp
No comments