Breaking News

Kituo cha Kijeshi Mlele Kinavyoandaa Maafisa na Askari wa Uhifadhi Kitaalamu




Na Mwandishi Wetu – Katavi

Kituo cha Mafunzo ya Kijeshi cha Mlele, kilichopo mkoani Katavi, kimeendelea kuwa kiungo muhimu katika kuimarisha uwezo wa askari na maafisa wa uhifadhi nchini kupitia mafunzo maalum ya kijeshi yanayotolewa kwa taasisi mbalimbali zilizo chini ya Wizara ya Maliasili na Utalii.

Mnamo tarehe 4 Julai 2025, ujumbe wa Menejimenti ya Wizara ya Maliasili na Utalii ulifanya ziara katika kituo hicho ili kujionea maendeleo ya mafunzo na namna kituo kinavyotekeleza majukumu yake. Ujumbe huo uliongozwa na Kamishna Msaidizi Mwandamizi (SACC), Fidelis Kapalata, ambaye pia ni Mkurugenzi wa Kitengo cha Uratibu wa Jeshi la Uhifadhi.

Kituo cha Mlele kimekuwa kikitoa mafunzo ya kijeshi kwa waajiriwa wapya kutoka taasisi za TANAPA, TAWA, TFS na Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA), ambapo muda wa mafunzo hutegemea nafasi ya ajira – aidha miezi mitatu au sita.

Katika ziara hiyo, ujumbe wa wizara ulitembelea maeneo mbalimbali ya kituo hicho ikiwemo mabweni ya wanafunzi, ofisi, viwanja vya mazoezi, zahanati, uwanja wa ndege mdogo, nyumba ya walimu na sehemu ya mapumziko, huku wakipata fursa ya kuzungumza na wakufunzi pamoja na wanafunzi.

Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Kamishna Kapalata alisema kuwa Kituo cha Mlele kimejipambanua kama taasisi bora katika kutoa mafunzo ya kijeshi kwa askari wa uhifadhi, jambo linalosaidia kuwajengea weledi, ujasiri na nidhamu ya kazi.

“Kila mwaka zaidi ya askari na maafisa 1,000 wanapokea mafunzo hapa. Lengo ni kuhakikisha wanaingia kazini wakiwa na uelewa sahihi wa mbinu za kisasa za uhifadhi na ulinzi wa rasilimali za taifa,” alisema Kapalata.

Kwa upande wake, Afisa Mwandamizi wa Uhifadhi (SCO), Šimon Msuva, alieleza kuwa kwa sasa kituo kina jumla ya wanafunzi 368 ambao wote ni ajira mpya kutoka Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), na wanatarajiwa kuhitimu baada ya miezi sita ya mafunzo.

“Mafunzo yanaendelea vizuri. Ndani ya kipindi cha miezi sita, vijana hawa watakuwa wameiva vya kutosha kulinda na kuhifadhi rasilimali zetu kwa weledi mkubwa,” alisema Msuva.

Kituo cha Mafunzo cha Mlele kilianza kutumika rasmi mwaka 2018, baada ya Wizara ya Maliasili na Utalii kubadilisha mfumo wa mafunzo kutoka kiraia na kuanzisha mfumo wa kijeshi kwa taasisi zake nne za uhifadhi, ili kuongeza ufanisi na uimara katika kutekeleza majukumu ya kulinda maliasili za taifa.

No comments