Breaking News

MALALA YOUSAFZAI : MWANAMKE ALIYEGEUZA RISASI KUWA SILAHA YA MABADILIKO YA ELIMU KWA MSICHANA


Malala Yousafzai akiwa na shujaa wake wa kwanza , baba yake mzazi Ziauddin Yousafzai 
ambaye wengi walimtaka anyamaze, lakini baba yake alimfundisha kusimama na leo hii nguvu ya sauti yake inatumika kuwatoa utumwani watoto wa kike kielimu.

Malala na mumewe Asser Malik ambaye anatajwa kama shujaa wa pili wa Malala anayeheshimu sauti ya mkewe na kumuimarisha kwa kila hatua.


Na Dotto Kwilasa: Julai 12 – Malala Day

Leo dunia inaadhimisha Malala Day, kumbukumbu ya kuzaliwa kwa msichana jasiri kutoka Pakistan aliyesimama kidete kutetea haki ya wasichana kupata elimu licha ya vitisho, risasi, na ukimya wa ulimwengu.

Hii ni siku ya kumkumbuka, kumshangilia, na kuendeleza harakati alizoanzisha akiwa bado na umri mdogo.

Mwanzo wa Safari Yake

Malala alizaliwa Julai 12, 1997 huko Mingora, Swat Valley, nchini Pakistan, Baba yake mzazi Ziauddin Yousafzai, alikuwa mwalimu, mwanaharakati, na mhamasishaji wa elimu aliyemlea Malala kwa misingi ya usawa, ujasiri na haki.

Alimkuza akiwa na imani kwamba msichana anaweza kuwa kiongozi kama mvulana, na ndiye aliyemhimiza Malala kusema hadharani kuhusu changamoto za elimu kwa wasichana.



Shambulio Lililozindua Dunia

Mnamo Oktoba 9, 2012, Malala alipigwa risasi kichwani na wanamgambo wa Taliban kwa sababu ya kampeni yake ya kutetea elimu ya mtoto wa kike.

Tukio hilo lililotokea akiwa ndani ya basi kurudi nyumbani kutoka shule liliishtua dunia nzima.

Baada ya tukio hilo, Malala alipelekwa Pakistan Army Hospital mjini Peshawar, kisha kuhamishiwa Uingereza kwa matibabu zaidi.

Gharama za safari na matibabu yake zilifadhiliwa na Serikali ya Uingereza, kupitia Waziri Mkuu wa wakati huo, David Cameron, kwa usaidizi wa Serikali ya Pakistan na Shirika la Afya Duniani.

Alilazwa katika Hospitali ya Queen Elizabeth, Birmingham, ambako alifanyiwa upasuaji na huduma maalum za kibingwa hadi kupona kikamilifu.



Malala Fund na Harakati za Kimataifa

Baada ya kupona, Malala hakuogopa ,aliinuka akiwa na nguvu mpya. Akiwa na baba yake kama mshauri na mshirika mkuu, alianzisha Malala Fund, shirika linalotetea haki ya elimu kwa wasichana duniani.

Leo hii, shirika hilo linaendesha miradi katika nchi kadhaa zikiwemo Nigeria, India, Afghanistan, Ethiopia na Pakistan, likisaidia mamilioni ya wasichana kupata fursa ya kwenda shule.

Tuzo ya Amani ya Nobel

Mwaka 2014, Malala alishinda Tuzo ya Amani ya Nobel, akiwa na umri wa miaka 17, na kuwa mshindi mdogo zaidi katika historia ya tuzo hiyo.

Alitunukiwa pamoja na Kailash Satyarthi wa India, kwa juhudi zao za kutetea haki za watoto. Tuzo hiyo ilikuwa heshima kubwa kwa ujasiri wake na msimamo thabiti katika kutetea elimu.



Elimu, Familia na Maisha Binafsi

Licha ya kuwa na majukumu mengi ya harakati za kimataifa, Malala alihitimu masomo yake katika Chuo Kikuu cha Oxford mwaka 2020, akisomea Falsafa, Siasa na Uchumi (PPE).

Baba yake, Ziauddin, aliendelea kuwa mlezi, rafiki na nguzo kuu katika maisha yake, akiambatana naye kwenye safari nyingi za kimataifa.

Mnamo Novemba 2021, Malala alifunga ndoa na Asser Malik, mmoja wa wakurugenzi wa bodi ya kriketi ya Pakistan (Pakistan Cricket Board).

Walikutana kwa njia ya kawaida kama marafiki, kabla ya mahusiano yao kuchanua na kuwa ndoa ya wazi na ya kuheshimiana.

Mpaka sasa, hawajaweka wazi kama watoto au lah , na wameamua kuweka maisha yao ya ndoa kuwa ya faragha zaidi huku wakiheshimu kazi na malengo ya kila mmoja.


Sauti ya Mabadiliko

Malala si jina tu, bali ni ishara ya msichana asiyeogopa kusema, aliyeamua kusimama kwa ajili ya wengine hata ikimgharimu maisha.

Leo tunapoadhimisha Malala Day, ni muda wa kujiuliza: Tumejifunza nini kutoka kwake? Tumefanya nini kama jamii kulinda haki ya elimu kwa kila mtoto, hasa wa kike?



Kwa maoni, ushauri tafadhali wasiliana na muandaaji wa makala hii kupitia dottokwilasa@gmail.com


from MALUNDE 1 BLOG https://ift.tt/PdFKJHx

No comments