Breaking News

Rais Samia aibadilisha Tabora, miradi ya Trilioni 15 yaleta mapinduzi ya kimaendeleo

-Hospitali 5, vituo vya afya 30 na zahanati 109 vyajengwa
-Shule za msingi zaongezeka hadi 990, sekondari 264
 -SGR na uwanja wa ndege wa Tabora waendelezwa kwa Bilioni 24
-Miradi 73 ya maji yakamilika, huduma ya maji vijijini yafikia 68.2%


 Na Mwanishi wetu Tanzania Yetu

Mkoa wa Tabora umeingia kwenye kipindi cha mageuzi makubwa ya kijamii na kiuchumi kufuatia utekelezaji wa miradi ya kimkakati yenye thamani ya zaidi ya shilingi trilioni 15 tangu mwaka 2021, chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Akizungumza jijini Tabora Julai 11, 2025, Mkuu wa Mkoa huo, Paulo Matiko Chacha, alisema kuwa rasilimali hizo zimeleta mabadiliko makubwa katika sekta za afya, elimu, miundombinu, kilimo, maji na mifugo, huku pato la mkoa likiongezeka kutoka trilioni 5.4 mwaka 2020 hadi trilioni 6.3 mwaka 2024. Aidha, pato la mtu mmoja mmoja limepanda kwa wastani wa asilimia 4.5.

Sekta ya Afya

Katika kipindi hicho, hospitali tano za wilaya zimekamilishwa, vituo vya afya 30 vimejengwa, na zahanati 109 zimekamilika. Bajeti ya dawa na vifaa tiba imeongezeka kutoka bilioni 4.2 hadi bilioni 9.8, na upatikanaji wa dawa umefikia asilimia 91.

Sekta ya Elimu

Mpango wa elimu bila malipo umeboresha upatikanaji wa elimu ambapo shule za msingi zimeongezeka kutoka 819 hadi 990, na sekondari kutoka 197 hadi 264. Serikali imetoa zaidi ya shilingi bilioni 146.6 kwa ujenzi wa madarasa, nyumba za walimu na miundombinu mingine muhimu, hatua iliyochangia ongezeko la ufaulu.

Miundombinu

Barabara za lami zimeongezeka, madaraja 116 yamejengwa, na taa za barabarani zimeongezeka kutoka 550 hadi 1,850. Aidha, ujenzi wa reli ya kisasa (SGR) unaendelea sambamba na ukarabati wa uwanja wa ndege wa Tabora kwa gharama ya zaidi ya shilingi bilioni 24.

Kilimo na Mifugo

Eneo la umwagiliaji limeongezeka hadi ekari 37,560, huku uzalishaji wa tumbaku ukiongezeka kutoka kilo milioni 29 hadi milioni 62. Majosho 95 yamejengwa na huduma za ugani zimeboreshwa kwa kupewa vifaa na usafiri wa kutosha.

Maji

Huduma ya maji imeimarika kwa kiwango kikubwa: Upatikanaji wa maji mijini umefikia asilimia 89.1 na vijijini asilimia 68.2. Miradi 73 ya maji imekamilika vijijini, huku idadi ya mabwawa ya maji ikiongezeka kutoka 10 hadi 13.

Mkuu huyo wa Mkoa amesema mafanikio haya ni ushahidi wa utekelezaji thabiti wa Ilani ya CCM na dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita ya kuhakikisha maendeleo jumuishi kwa Watanzania wote.

 

No comments