SERIKALI YATULIZA MIGOGORO MARA, YAWEZESHA JAMII KUSTAWI KUPITIA UTAWALA WA RASILIMALI
Na Dotto Kwilasa,Dodoma
Mkuu wa Mkoa wa Mara Kanali Evans Alfred Mtambi amesema Mkoa huo umekuwa mfano bora wa usalama na utulivu, hali inayochangia moja kwa moja maendeleo endelevu katika sekta mbalimbali za kiuchumi na kijamii.
Amesema kuwa katika kipindi cha miaka minne ya uongozi wa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, usalama umeimarika sana na migogoro ya ardhi kupungua kwa kiasi kikubwa.
Akizungumza na waandishi wa Habari kwenye ukumbi wa Idara ya Habari-MAELEZO leo July 18,2025 Jijini Dodoma amesema Katika suala la migogoro ya ardhi, Serikali kupitia halmashauri zimetumia shilingi bilioni 2.8 kwa ajili ya zoezi la kupanga, kupima na kumilikisha ardhi.
Amefafanua kuwa hatua hiyo imepunguza migogoro kutoka 964 mwaka 2020 hadi migogoro 125 mwaka 2025. Usalama wa ardhi umeongeza amani na kuleta ushawishi mzuri kwa uwekezaji katika sekta za kilimo, biashara, na madini.
Pia,ameeleza kuwa Mkoa wa Mara una hifadhi kubwa ya wanyamapori ikiwemo Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, ambayo ni mojawapo ya hifadhi muhimu zaidi Afrika na duniani.
Amesema Serikali itaendelea kuweka usimamizi bora wa eneo hilo, kuhakikisha wanyama na wakazi wanaishi kwa mshikamano, huku ikizingatia haki za wananchi na malipo ya fidia kwa wale waliokamatwa maeneo ya hifadhi.
Amesema Malipo ya fidia ya shilingi bilioni 59.52 kwa wananchi wa Kata ya Nyatwali kwa ajili ya maeneo yaliyochangia utunzaji wa ikolojia na usalama wa wanyamapori, yameimarisha usalama wa maisha ya wananchi na kupunguza mikwaruzano iliyokuwa ikijitokeza mara kwa mara.
Akizungumzia huduma za usalama katika Mkoa wa Mara, amesema zimeimarika kwa ujenzi wa majengo ya ofisi za polisi, vituo vya usalama na mahakama hali inayochangia kupunguza uhalifu na kuwezesha usimamizi bora wa rasilimali na amani ya wananchi.
Kanali Mtambi pia ameeleza kuwa usalama wa mazingira na usimamizi bora wa rasilimali za asili umesaidia kukuza utalii na hivyo kuongeza kipato cha mkoa. Mradi wa ujenzi wa uwanja wa ndege wa Musoma na miundombinu ya barabara ni sehemu ya mikakati ya kukuza utalii wa hifadhi.
from MALUNDE 1 BLOG https://ift.tt/aGx2r5W
No comments