TANESCO yachochea matumizi ya Nishati Safi kwa kutoa majiko ya umeme Sabasaba
Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) limechukua hatua ya kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia kwa kugawa majiko ya umeme kwa wananchi waliotembelea banda lao katika Maonesho ya 49 ya Biashara ya Kimataifa maarufu kama Sabasaba, yanayoendelea jijini Dar es Salaam.
Akizungumza leo Julai 7, 2025, katika viwanja vya maonesho hayo, Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Bw. Lazaro Twange, amesema wananchi waliotembelea banda hilo wamepata elimu kuhusu faida na umuhimu wa kutumia nishati safi, sambamba na kushiriki maswali yaliyowawezesha kujishindia majiko ya umeme kama zawadi.
"Rais Samia Suluhu Hassan amekuwa mstari wa mbele kuhimiza matumizi ya nishati safi. Sisi TANESCO tunatekeleza maelekezo hayo kwa vitendo kwa kutoa elimu na kugawa majiko ya umeme yanayotumia chini ya Unit moja ya umeme hadi chakula kiive," amesema Twange.
Ameongeza kuwa, wananchi walioshiriki shindano la maswali katika banda lao walipata fursa ya kujishindia majiko hayo na amewataka wawe mabalozi wa matumizi ya nishati safi kwa familia na jamii zao.
Kwa upande wake, Kaimu Meneja Mkuu wa Kampuni ya Ujenzi na Ukarabati wa Miundombinu ya Usafirishaji na Usambazaji wa Umeme (ETDCO), Bw. Sadock Mugendi, amesema kampuni hiyo imekuwa mstari wa mbele katika kusambaza umeme vijijini. Amesema hivi karibuni wamekamilisha mradi mkubwa wa kusafirisha umeme kutoka Tabora mjini hadi Katavi, umbali wa kilomita 383 kwa msongo wa kilovolt 132.
"Mradi huu ni mafanikio makubwa kwa serikali na wananchi. Pia tunaendelea na miradi mingine katika maeneo ya Mbeya na Katavi kuhakikisha umeme unawafikia Watanzania wengi zaidi," amesema Mugendi.
Naye Meneja Mkuu wa Kampuni ya Uendelezaji wa Jotoardhi Tanzania (TGDC), Bw. Mathew Mwangomba, amesema kampuni yao inaendelea na uthibitishaji wa vyanzo vya nishati ya jotoardhi mkoani Mbeya, hasa katika eneo la Mbozi.
"Katika eneo hilo, tumehakiki uwezo wa kuzalisha megawati 70 ambazo zitachangia katika Gridi ya Taifa. Tunawaalika wawekezaji wa ndani na nje kushirikiana nasi katika kuendeleza sekta hii ya nishati mbadala," amesema Mwangomba.
No comments