Breaking News

TBS yasisitiza uhakiki sahihi wa vipimo kwa taasisi za umma na binafsi



Na Mwandishi Wetu - Tanzania Yetu Blog na Gazeti

Shirika la Viwango Tanzania (TBS) limewahimiza wadau kutoka sekta mbalimbali, zikiwemo taasisi za serikali, hospitali, viwanda na miradi ya ujenzi, kuchangamkia huduma ya uthibitishaji wa mifumo na uhakiki wa vipimo inayotolewa na shirika hilo kwa gharama nafuu, ili kuhakikisha ubora na usahihi katika utoaji wa huduma na uzalishaji.

Akizungumza kwenye Maonesho ya 49 ya Biashara ya Kimataifa yanayoendelea katika viwanja vya Mwalimu Nyerere, Barabara ya Kilwa jijini Dar es Salaam, Meneja wa Uhusiano na Masoko wa TBS, Bi. Gladness Kaseka, alisema shirika hilo lina uwezo wa kutoa huduma hizo kwa viwango vya kimataifa, tofauti na ilivyokuwa zamani ambapo taasisi nyingi ziliwalazimika kutafuta huduma hizo nje ya nchi.

“TBS tunayo ithibati ya kimataifa ya kutoa huduma za System Certification, na tunakaribisha taasisi zote — za serikali na binafsi — kuja kupata huduma hii hapa nchini badala ya kutegemea makampuni ya nje,” alisema Kaseka.

Kwa upande mwingine, Bi. Kaseka alisisitiza umuhimu wa huduma ya metrology (ugezi), hususan kwa hospitali, miradi ya ujenzi, na viwanda. Alisema uhakiki wa vipimo unasaidia kuondoa mkanganyiko unaojitokeza kwa wateja wanapopata matokeo tofauti kutoka vituo mbalimbali vya huduma.

“Watoa huduma wanapopoteza imani ya wateja kwa sababu ya vipimo visivyo sahihi, athari huathiri taasisi nzima. TBS ipo kwa ajili ya kuhakikisha vifaa vyao vinapimwa kwa usahihi na vinatoa majibu ya kuaminika,” aliongeza.

Alifafanua kuwa huduma ya ugezi hutolewa kwa kuwafuata wadau kwenye maeneo yao ya kazi, iwe hospitalini au viwandani, na inahusisha uhakiki wa vifaa vinavyotumika katika maabara na uzalishaji.

Aidha, Bi. Kaseka alisema kuwa mwitikio wa taasisi kujitokeza kupata huduma hiyo ni mkubwa, lakini aliwahimiza zaidi hospitali, zikiwemo zahanati, kutojisahau kwa kudhani kuwa ni ndogo kwani hata huduma ndogo inaweza kuwa na athari kubwa kwa maisha ya mtu.

“Tunaamini kila mtoa huduma anapaswa kuwa na vipimo sahihi ili kuepuka kupoteza wateja na kulinda uwekezaji pamoja na ajira zilizopo,” alisisitiza.

Kwa sasa, TBS imeanza kutembelea hospitali mbalimbali kwa ajili ya kufanya ugezi, lakini pia imetoa wito kwa taasisi ambazo bado hazijatembelewa kufika moja kwa moja TBS au banda lao kwenye maonesho ya Sabasaba kupata maelezo na huduma hiyo muhimu.









No comments