Breaking News

Tume ya Madini yaanika dhamira mpya ya Tanzania kuvunja vikwazo vya uwekezaji kimataifa


Na Mwandishi Wetu – Dar es Salaam

Katika kile kinachoonekana kama hatua mpya ya kuamsha nguvu ya kiuchumi kupitia madini, Serikali kupitia Tume ya Madini imetangaza mpango mahsusi wa kuongeza kasi ya kuvutia wawekezaji ndani na nje ya mipaka ya nchi. Hatua hii imeelezwa kuwa ni sehemu ya mkakati wa taifa kujitangaza kimataifa kama kitovu cha biashara ya madini Afrika Mashariki.

Akizungumza katika Maonesho ya 49 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (DITF), Mwenyekiti wa Tume hiyo, Dkt. Janet R. Lekashingo, alisema ipo haja ya Tanzania kuondoka katika upweke wa kimkakati na kufungua milango kwa majukwaa mapya ya kimataifa yenye fursa za uwekezaji mkubwa.

“Tanzania haiwezi kuendelea kuwa mfuatiliaji wa mwelekeo wa soko la madini duniani, tunahitaji kuwa sehemu ya waamuzi. Dunia inapaswa kufahamu hazina tuliyonayo—kutoka utafiti, uongezaji thamani hadi biashara ya kimataifa ya madini,” alisema Dkt. Lekashingo.

Katika ziara hiyo, Dkt. Lekashingo aliambatana na Makamishna Eng. Theonestina Mwasha na Dkt. Theresia Numbi ambapo walipata fursa ya kuzungumza na wadau wa sekta hiyo, huku wakikagua utekelezaji wa majukumu ya taasisi zilizo chini ya Wizara ya Madini.

Wizara hiyo imeweka wazi taasisi zake ikiwemo Tume ya Madini, Mpango wa TEITI, Kituo cha TGC, na STAMICO, kama njia ya kutoa elimu, kuvutia ubia na kuelezea mafanikio yaliyopatikana kutokana na mageuzi ya sera.

Katika kuonesha ushirikiano wa kijamii, Dkt. Lekashingo alitembelea pia banda la “Made in Tanzania” na Mfuko wa Fursa Sawa kwa Wote (EOTF), jambo lililotafsiriwa kama msimamo wa kisera wa kuunga mkono wanawake na wajasiriamali wa Kitanzania katika mnyororo wa thamani wa rasilimali.

Mkurugenzi Mkuu wa TanTrade, Bi Latifa M. Khamis, alisema ushiriki wa Tume ya Madini katika maonesho hayo unatoa ujumbe mzito kwa wawekezaji kuwa Tanzania iko tayari kushindana kisoko.

“Tunahitaji kujenga taswira mpya ya Tanzania. Sio tu kama nchi ya rasilimali, bali kama mshirika salama wa uwekezaji wa kimataifa,” alisema Bi Latifa.

Maonesho ya mwaka huu, yaliyovuta zaidi ya washiriki 3,000 kutoka mataifa mbalimbali, yanatajwa kuwa jukwaa mahsusi la Tanzania kujiuza upya kibiashara katika zama hizi za ushindani mkubwa wa kiuchumi.

Ziara ya Dkt. Lekashingo imeonekana kuwa ni ujumbe wa wazi kuwa Serikali haitaki tena nafasi ya pili, bali inataka nafasi ya kuongoza bara la Afrika katika biashara ya madini kwa njia ya wazi, jumuishi na yenye mafanikio kwa wananchi wake.

No comments