Tanzania yatimiza lengo la watalii milioni 5 – Waziri Pindi Chana
Na Mwandishi Wetu – Dar es Salaam
Na Mwandishi Wetu – Dar es Salaam
Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana (Mb), ameipongeza Wizara ya Maliasili na Utalii pamoja na wadau wa sekta hiyo kwa kufanikisha azma ya Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya kufikisha watalii milioni tano nchini, kama ilivyoainishwa katika dira ya maendeleo ya chama hicho.
Akizungumza katika uzinduzi wa Siku ya Ngorongoro (Ngorongoro Day), uliofanyika sambamba na Maonesho ya 49 ya Biashara ya Kimataifa maarufu kama Sabasaba, Dkt. Chana alisema kuwa mafanikio hayo ni ushahidi wa jitihada za pamoja na uongozi madhubuti ndani ya sekta hiyo.
“Niwapongeze sana watendaji wenzangu wa Wizara ya Maliasili na Utalii pamoja na wadau wote wa sekta hii. Ilani ya CCM ilielekeza tufikishe watalii milioni tano, na leo hii tunatembea kifua mbele kwa kuwa tumefikia lengo hilo,” alieleza Dkt. Chana kwa fahari.
Aidha, Waziri Chana alitumia fursa hiyo kuipongeza Mamlaka ya Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro (NCAA) kwa mafanikio makubwa ya mapato, ambapo hadi kufikia sasa imekusanya shilingi bilioni 269.9, ikilinganishwa na lengo la awali la bilioni 230 kwa mwaka wa fedha 2024/25.
Akitoa maelezo kuhusu maadhimisho hayo, Meneja wa Huduma za Utalii na Masoko wa NCAA, Bi. Mariam Kobelo, alisema kuwa lengo kuu la Siku ya Ngorongoro ni kuunga mkono juhudi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, katika kutangaza vivutio vya utalii vya Tanzania na kuongeza idadi ya wageni kutoka nje ya nchi.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), Bw. Ephraim Mafuru, alieleza kuwa Bodi hiyo itaendelea kushirikiana kwa karibu na taasisi nyingine zilizo chini ya Wizara ya Maliasili na Utalii kuhakikisha kuwa sekta hiyo inaendelea kukuza pato la taifa kupitia ongezeko la watalii na mapato yanayotokana na utalii.
“Tutaendelea kushirikiana kwa karibu ili kuhakikisha siyo tu idadi ya watalii inaongezeka, bali pia mchango wa sekta hii kwenye uchumi wa taifa unazidi kuwa mkubwa,” alisema Mafuru.
Maadhimisho ya Siku ya Ngorongoro yameendelea kuonesha dhamira ya serikali ya kuboresha na kulinda rasilimali za kitalii nchini, huku yakichagizwa na juhudi endelevu za kukuza sekta hiyo kimataifa.
No comments