Breaking News

WAHITIMU WA DARASA LA SABA 2002 MITWERO WAKABIDHI MADAWATI, WAMEOMBA WADAU KUJITOKEZA KUSAIDIA

baadhi ya wahitimu wa darasa la saba mwaka 2002 wakiwa pamoja na walimu na wanafunzi wa shule ya msingi Mitwero mkoani Lindi baada ya kukabidhi madawati shuleni 

Na Regina Ndumbaro-Lindi 

Baadhi ya wahitimu wa darasa la saba mwaka 2002 kutoka Shule ya Msingi Mitwero, iliyopo Kata ya Rasibula, Manispaa ya Lindi, wamekabidhi msaada wa madawati 8 yenye thamani ya Shilingi 780,000 kwa shule yao ya zamani. 

Wahitimu hao walikabidhi madawati hayo kama njia ya kurudisha shukrani kwa jamii na kusaidia kutatua changamoto ya uhaba wa madawati shuleni hapo. 

Mwenyekiti wa umoja huo, Mosses Verisi, amesema wameanza na kidogo lakini wana dhamira ya kuendelea kusaidia zaidi kila mwaka.

Mwalimu  mkuu  msaidizi wa shule ya msingi Mitwero, Amina Mohamedi, amesema shule hiyo ilikuwa na uhaba wa madawati 45 na msaada huo wa madawati 8 umepunguza pengo hilo hadi 37. 

Amewataka wahitimu wengine pamoja na wadau mbalimbali kujitokeza kusaidia ukarabati wa madarasa chakavu ambayo yanavuja, akisisitiza kuwa shule hiyo bado inakabiliwa na changamoto nyingi za miundombinu.

Kwa upande wa wanafunzi wa sasa, akiwemo Yasini Steven na Agnes Raymond, wameeleza furaha yao kwa kupokea madawati hayo, wakisema yatasaidia kupunguza msongamano darasani na kuongeza hamasa ya kuhudhuria masomo. 

Wametoa wito wa kupatiwa msaada zaidi kama vitabu na vifaa vingine vya kufundishia

Akizungumza wakati wa hafla ya makabidhiano, Mkuu wa Wilaya ya Lindi, Victoria Mwanziva, amewapongeza wahitimu hao kwa moyo wao wa kujitolea na kuwasihi wahitimu wengine wa shule za serikali kufuata mfano huo.

Pia Kaimu Afisa Elimu Msingi na Awali, Selemani Mgeleka, ameahidi kushirikiana na wadau hao na kuwataarifu pindi shughuli za ukarabati zitakapoanza ili waweze kushiriki kikamilifu.


Baadhi ya wanafunzi wakiwa wamekaa juu ya madawati hayo baada ya kuletwa na wanafunzi waliohitimu darasa la saba mwaka 2002 shuleni hapo 






from MALUNDE 1 BLOG https://ift.tt/mkK13lZ

No comments