Dar es Salaam – Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ametoa maagizo kwa waendeshaji wa awamu ya pili ya Mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka (BRT-2) kuhakikisha wanakamilisha taratibu zote zilizobaki haraka, ili huduma ianze kutolewa ndani ya muda mfupi.
Akiwa katika ziara ya ukaguzi wa mabasi mapya na miundombinu yake leo (Agosti 13, 2025), Majaliwa alisisitiza kuwa kazi ifanyike usiku na mchana kwenye vituo vikuu vya Mbagala Rangi Tatu na Gerezani, pamoja na ujenzi wa kituo cha kujazia gesi.
"Mradi huu utaongeza ufanisi wa usafiri wa umma na kutoa huduma za kisasa, salama na za haraka kwa wakazi wa Dar es Salaam. Tunataka utekelezwe kikamilifu na kwa wakati," alisema Majaliwa.
Alimtaka Mkurugenzi Mkuu wa kampuni ya Mofat, Mohammed Kassim, kuharakisha uondoaji wa mabasi 99 yaliyopo bandarini, ili kuanza huduma mapema. Aidha, alisisitiza kuwa mfumo wa tiketi uwe wa kielektroniki badala ya karatasi, kwa lengo la kudhibiti mapato.
Waziri Mkuu pia aliwahimiza Watanzania kuchangamkia ajira zitakazotokana na mradi huo, hasa madereva, akiwashauri kujiandaa kupitia mafunzo ya Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT).
Kuhusu kituo cha kujazia gesi kinachojengwa na kampuni ya Lake Oil, Majaliwa alitaka mitambo isimikiwe mara moja ili huduma ianze.
Katika ziara hiyo alifuatana na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) William Lukuvi, Naibu Waziri Ofisi ya Rais (TAMISEMI) Zainab Katimba, Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Dkt. Jim Yonazi, pamoja na viongozi wa LATRA, DART na NIT.
