Mauaji ya Waandishi Gaza; WAPC Yashutumu Israel, Yataka Uchunguzi wa Kimataifa


  • Waandishi 6 wauawa kwa shambulio la anga karibu na Hospitali ya Al-Shifa
  • Zaidi ya wanahabari 240 wameuawa Gaza tangu Oktoba 2023
  • Umoja wa Mataifa wataka uchunguzi huru wa kimataifa

Na Mwandishi wetu - Dar es Salaam, Tanzania 

Shirikisho la Baraza la Vyombo vya Habari Duniani (World Association of Press Councils (WAPC) limeilaani vikali Israel kwa kile linachokiita mauaji yaliyolengwa ya waandishi wa habari mjini Gaza, likiutaja kuwa ni uvunjifu mkubwa wa haki za binadamu na uhuru wa habari duniani.

Tarehe 10 Agosti 2025, shambulio la anga la Israel lilipiga hema la waandishi wa habari karibu na Hospitali ya al-Shifa, Gaza City, na kuua waandishi watano wa Al Jazeera  Anas al-Sharif, Mohammed Qreiqeh, Ibrahim Zaher, Mohammed Noufal na Moamen Aliwa pamoja na mwandishi wa kujitegemea Mohammad al-Khaldi.

WAPC imesema waandishi hao walikuwa waangalizi huru waliokuwa wakiripoti ukweli na kutoa sauti kwa raia wasio na nafasi ya kujieleza, na si wapiganaji kama ilivyodaiwa na jeshi la Israel.

Tangu Oktoba 7, 2023, zaidi ya waandishi wa habari na wafanyakazi wa vyombo vya habari 242 wengi wao Wapalestina wameuawa katika mashambulizi yanayohusiana na mzozo wa Gaza. WAPC imeutaja kipindi hiki kama cha mauaji mabaya zaidi kwa wanahabari katika historia ya kisasa, na kuongeza kuwa hakuna mzozo mwingine umewahi kushuhudia idadi kubwa ya vifo vya wanahabari katika muda mfupi kiasi hiki.

Mashirika ya kimataifa yameendelea kushutumu kile kinachoelezwa kama mauaji ya mfumo dhidi ya wanahabari, uharibifu wa miundombinu ya vyombo vya habari na vizuizi dhidi ya taarifa huru. WAPC imesisitiza kuwa vitendo hivyo ni uvunjaji wa moja kwa moja wa sheria za kimataifa za kibinadamu na vinatishia demokrasia ya dunia nzima.

Rais wa WAPC, David Omwoyo, amesema shirikisho hilo linaunga mkono wito wa Umoja wa Mataifa wa kufanyika kwa uchunguzi wa kina, wa haraka na huru wa kimataifa ili kuwawajibisha wote waliohusika. Amezitaka pande zote katika mzozo wa Gaza kuheshimu ulinzi wa wanahabari chini ya Mikataba ya Geneva na kusitisha mara moja mashambulizi dhidi yao.

“Hakuna nguvu za ghasia zitakazoweza kuinyamazisha kalamu,” amesema Omwoyo. “Ukweli utashinda.”

 
Mwandishi Anas al-Sharif alikuwa miongoni mwa wafanyakazi watano wa Al Jazeera waliouawa na shambulio la Israel huko Gaza.

Post a Comment

Previous Post Next Post