Breaking News

POLISI JAMII FITNESS CENTER SHINYANGA YAZINDUA MARATHON KUKUSANYA MILIONI 520 KWA AJILI YA PIKIPIKI ZA KUIMARISHA USALAMA


Na Mwandishi wetu - Malunde 1 blog

Kikundi cha mazoezi cha Polisi Jamii Fitness Center (PJFCS) kilichopo Manispaa ya Shinyanga kimezindua rasmi kampeni ya mbio za marathon zenye umbali wa kilomita 5, 10 na 21 pamoja na vifaa mbalimbali vitakavyotumika, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kukusanya Shilingi milioni 520 kwa ajili ya ununuzi wa pikipiki zitakazotumiwa na maafisa wa Polisi Jamii katika kuimarisha utendaji wao wa kazi.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo uliofanyika Oktoba 25,2025, Mwenyekiti wa mbio hizo, Ignas Banyema, ameupongeza uongozi wa serikali ya mkoa wa Shinyanga kwa kuendelea kushirikiana nao katika kufanikisha malengo ya kikundi hicho, huku akiomba msaada wa kupata wadhamini zaidi ili kufikia lengo lililowekwa.

“Mheshimiwa Mkuu wa Wilaya tunakushukuru sana kwa kufika hapa leo kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wetu wa Shinyanga Mheshimiwa Mboni Mhita. Umezindua rasmi mpango wa Shinyanga Marathon pamoja na vifaa vitakavyotumika. Tunaomba serikali ya mkoa iendelee kutushika mkono katika hatua zote za kupata wadhamini, kwani lengo letu ni kukusanya Shilingi milioni 520 ili kufanikisha ununuzi wa pikipiki kwa askari wetu wa Polisi Jamii,” amesema Banyema.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Wakili Julius Mtatiro, aliyemwakilisha Mkuu wa Mkoa, ameipongeza PJFCS kwa ubunifu na dhamira njema waliyoionesha kupitia kampeni hiyo, huku akiahidi kuwa serikali ya mkoa itaendelea kuwaunga mkono.

“Serikali ya mkoa itaendelea kuwa bega kwa bega nanyi, kwani malengo yenu ni mazuri na yenye manufaa makubwa kwa Polisi Jamii na jamii kwa ujumla. Endeleeni na jitihada hizi, kwani mazoezi ni afya na pia yanaunganisha watu. Hata hivyo, niwakumbushe kuendelea kushiriki ipasavyo katika zoezi la uchaguzi mkuu,” amesema Wakili Mtatiro.

Kikundi cha Polisi Jamii Fitness Center kimekuwepo kwa zaidi ya miaka 10, kikiwa na washiriki zaidi ya 200, kikijikita katika kuhamasisha mazoezi, afya, na ushirikiano baina ya wananchi na Jeshi la Polisi.

Kaulimbiu ya mwaka huu ni:“Kimbia kwa Afya, Imarisha Usalama wa Raia na Mali Zao.”































from MALUNDE 1 BLOG https://ift.tt/gsqzOMb

No comments