Breaking News

VIONGOZI WA DINI NA WAANDISHI WA HABARI WATAKIWA KUWA MABALOZI WA AMANI KUELEKEA UCHAGUZI MKUU



Na Mwandishi wetu, Iringa

Viongozi wa dini na madhehebu mbalimbali nchini, pamoja na waandishi wa habari, wametakiwa kutumia nafasi zao kwa hekima katika kuhimiza amani, umoja na maridhiano ya kitaifa, hususan katika kipindi hiki cha kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025, ili kuepusha mifarakano na migawanyiko miongoni mwa Watanzania.

Wito huo umetolewa leo, Alhamisi Oktoba 9, 2025, mkoani Iringa, katika warsha ya siku moja iliyoandaliwa na Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA) kwa kushirikiana na waandishi wa habari na viongozi wa dini kutoka madhehebu mbalimbali mkoani humo.

Mwezeshaji wa warsha hiyo, Uzima Justine, alisema huu ni wakati muhimu kwa viongozi wa dini na wanahabari kutumia kalamu, mimbar na majukwaa yao kuhubiri amani na umoja badala ya kutoa maneno yanayoweza kuchochea chuki au migawanyiko.

“Chochote kisichounganisha watu na kuleta amani si cha kweli,” alisema Uzima, akisisitiza kuwa wajibu wa viongozi wa dini ni kujenga maridhiano na upendo wakati wote, hasa katika kipindi nyeti cha uchaguzi.


Kwa upande wake, Mratibu wa warsha hiyo, Omary Ibrahim, ambaye ni Afisa Miradi wa BAKWATA Makao Makuu, alisema lengo kuu la kikao hicho ni kuwaongezea washiriki uelewa kuhusu nafasi yao katika kulinda amani kupitia maneno, maandiko na matendo yao.

 “Tupo Iringa na tumewakutanisha waandishi wa habari pamoja na viongozi wa dini — hawa ni watu wenye ushawishi mkubwa wanaoweza kujenga au kubomoa. Tunawajengea uwezo ili wakatoe elimu sahihi kwa wananchi na kuzingatia misingi ya ukweli,” alisema Omary.

Ameongeza kuwa wakati mwingine uhuru wa kukusanya na kusambaza habari hutumiwa vibaya, jambo linaloweza kuleta mkanganyiko kwa jamii na kuhatarisha amani ya nchi.

 “Ni muhimu kutumia kalamu na minbar kwa kuelimisha, sio kugawa,” alisisitiza.


Katika warsha hiyo, washiriki waliitaka serikali, taasisi za dini na vyombo vya habari kuimarisha ushirikiano katika kutoa elimu ya uraia, kuhimiza umoja wa kitaifa, na kupinga taarifa au mafundisho yenye mwelekeo wa kuchochea migawanyiko.

 “Amani ni urithi wa taifa; tusiiache ipotee kwa maneno yetu au taarifa zisizo sahihi,” ulisema ujumbe wa pamoja wa washiriki hao.




from MALUNDE 1 BLOG https://ift.tt/yGMVPL9

No comments