Breaking News

MWENDOKASI ZA MBAGALA KUREJEA - CHALAMILA AKIHAMASISHA AMANI, UPENDO NA MSHIKAMANO



Na Mwandishi wetu, Dar

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mhe. Albert Chalamila, ameagiza kurejeshwa kwa huduma ya mabasi ya mwendokasi katika kituo cha Mbagala kuanzia Alhamisi ya Novemba 20, 2025, ikiwa ni sehemu ya hatua za serikali kurejesha huduma kwa wananchi kufuatia vurugu zilizojitokeza baada ya uchaguzi mkuu wa Oktoba 29, 2025.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Jumanne Novemba 18, 2025, wakati wa ziara ya kukagua baadhi ya vituo vilivyoharibiwa katika Wilaya ya Temeke, Mhe. Chalamila amesema ni wajibu wa serikali wa kuhakikisha wananchi wanapata huduma muhimu bila kuchelewa, hasa katika maeneo yaliyoathirika zaidi kama eneo hilo la Mbagala.

Agizo hilo linakuja kufuatia ombi la Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Mhe. Sixtus Mapunda ambaye aliomba baadhi ya huduma muhimu, zikiwemo za usafiri wa mwendokasi, kurejeshwa kwa haraka ili kupunguza usumbufu kwa wakazi wa eneo hilo.

Aidha, Mkuu huyo wa Mkoa ameeleza kuwa licha ya uharibifu mkubwa wa vituo vya mwendokasi, hakuna shule yoyote iliyoripotiwa kuchomwa au kuharibiwa kwenye vurugu na ghasia za Oktoba 29, 2025, akisisitiza kuwa serikali itaendelea na tathmini ya uharibifu wa mali ya umma na watu binafsi ili kuweka mkakati madhubuti wa urejeshaji wa huduma hizo.

Chalamila pia ametoa wito kwa wananchi wa Dar es Salaam kuwa watulivu na kudumisha amani, mshikamano na upendo miongoni mwao. Amesema ni muhimu kwa jamii kutoangalia migogoro ya kisiasa kwa mtazamo wa juujuu, kwani inaweza kuchochea mgawanyiko wa kitaifa na kutoa mianya kwa maadui wa taifa kuivuruga amani, akisisitiza kuwa Dar es Salaam ina nafasi kubwa ya kuwa mfano wa utulivu na mshikamano, hivyo ni wajibu wa wakazi wake kuwa na subira, kuvumiliana na kuweka mbele maslahi ya umma.




from MALUNDE 1 BLOG https://ift.tt/A36Iqa0

No comments