TAHADHARI: ‘UTANDAWAZI NI CHUI’, TUJILINDE NA UTEKAJI WA AKILI NA FIKRA

Katika siku za hivi karibuni, kumekuwa na mjadala mzito kwenye mitandao ya kijamii nchini, ambapo baadhi ya watu wameonekana kushabikia vitendo vya mataifa makubwa, hususan Marekani, kuvamia mataifa mengine huru na kuwaondoa madarakani viongozi waliochaguliwa na wananchi wao.
Hali hii imeibua maswali mazito kuhusu uzalendo wa baadhi ya Watanzania na uelewa wao wa siasa za kimataifa (Geopolitics), huku ikionekana wazi kuwa uvamizi huo mara nyingi hulenga kulinda maslahi ya taifa mvamizi na si demokrasia kama inavyodaiwa.
Wachambuzi wa mambo wameonya kuwa, kutoa sapoti kwa mataifa makubwa yanapovunja sheria za kimataifa ni ishara ya "kutekwa kiakili." Katika muktadha huu, msanii na mshairi wa kisasa, Lwaga Mwambande, ameibuka na shairi lenye tahadhari nzito kwa jamii, akisisitiza kuwa utandawazi na teknolojia vimekuwa silaha mpya zinazotumiwa na "adui" kuteka fikra za watu bila wao wenyewe kujua.
Sanaa ya Mwambande na Utekaji wa Akili
Kupitia shairi lake maarufu la “Tunatekwa Hatujui”, Mwambande anatumia lugha ya picha kuonya jinsi ambavyo binadamu wa sasa anavyopoteza uwezo wa kufanya maamuzi huru. Anasema:
“Tunatekwa hatujui, tunategwa hatujui, tunashikwa hatujui, akili ituingie.”
Mshairi huyu anaufananisha utandawazi na "chui" mwenye makucha ya "buibui," akimaanisha kuwa ni mfumo uliotengenezwa kwa ufundi mkubwa wa kunasa akili za watu kupitia runinga, vishikwambi, na simu janja. Kwa mujibu wa Mwambande, wakati watu wakisherehekea picha, vichekesho, na michezo ya kubashiri (kubeti) kwenye mitandao, wanashindwa kutambua kuwa muda wao na uwezo wao wa kufikiri unateketezwa.
Jiopolitiki na Maslahi ya Mataifa Makubwa
Kushabikia uvamizi wa taifa huru kwa kisingizio cha kuleta mabadiliko ni kukosa uelewa wa historia. Wanataaluma wanabainisha kuwa uvamizi wa kijeshi na kuingilia siasa za mataifa mengine mara nyingi hufuatiwa na uporaji wa rasilimali na kudhoofisha uhuru wa kiuchumi.
Mwambande anatoa tahadhari kuwa "adui" huja kwa namna ambayo hatumtambui, tukijiona hatuugui wakati akili zetu zimeshazidiwa. Katika beti zake, anauliza:
“Kaenda huko adui, ajua hatutambui, twaona hatuugui, akili ituingie.”
Hii ni sawia na wale wanaoshangilia machafuko yanayopandikizwa na mataifa ya nje, wakidhani ni ukombozi, kumbe ni mtego wa kutawaliwa upya kiakili na kiuchumi.
Wito wa Uzalendo na Fikra Huru
Ili kukabiliana na changamoto hizi, makala za wanataaluma na mashairi ya Mwambande yanapendekeza kuimarisha elimu ya fikra huru. Ni lazima Watanzania wajifunze kulinda maslahi ya ndani na kuhifadhi tamaduni zao badala ya kuwa mashabiki wa kila kinachotoka nje, hata kama kina madhara kwa amani ya dunia.
Mwambande anahitimisha kwa uchungu akisema kuwa tunacheka na vichekesho visivyotatua shida zetu, na kusoma vitabu hatutaki, jambo linalotufanya tubaki tukiwa "hatukui."
Ni wazi kuwa, katika ulimwengu huu wa utandawazi, silaha kubwa ya kujilinda si bunduki pekee, bali ni "Akili." Kama taifa, tunapaswa kuwa macho na wale wanaotaka kutugawa na kutufanya tushabikie uharibifu wa mataifa mengine, kwani gharama ya kupoteza amani na uhuru ni kubwa, na mara nyingi huanza kwa kutekwa kwa akili.
from MALUNDE 1 BLOG https://ift.tt/oTpPAaZ
No comments