NEMC YAKIFUNGA KIWANDA CHA HOOTA KWA KUTOKUZINGATIA TARATIBU ZA KIMAZINGIRA
Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira NEMC Leo Februari 9, 2026 limekifunga kiwanda cha urejelezaji wa taka za plastiki cha HOOTA kilichopo Kata ya Vikindu Mkoani Pwani kutokana na kutekeleza shughuli zake kinyume na taratibu za kimazingira.
Akizungumza mara baada ya timu ya wataalamu wa Mazingira kutoka NEMC kukagua kiwanda hicho, Meneja Utekelezaji wa Sheria (NEMC) Mhandisi Luhuvilo Mwamila ameeleza changamoto zilizobainika katika kiwanda hicho ikiwa ni Pamoja kuanzisha kiwanda bila kufanya Tathmini ya Athari kwa Mazingira (TAM) na kutokuwa na cheti cha Mazingira, kuanzisha kiwanda katikati ya makazi ya watu hivyo kuhatarisha usalama wa wakazi wa maeneo hayo, pia kukosa teknolojia madhubuti ya kudhibiti hewa ya kemikali inayosababishwa na uendeshaji wa kiwanda hicho, kukosekana kwa vifaa kinga kwa wafanyakazi na utiririshaji wa maji taka kwenye makazi ya watu bila kuyatibu.
Ameeleza kuwa, awali NEMC ilikagua kiwanda hicho na kutoa maelekezo ambayo kiwanda hicho kinatakiwa kuzingatia lakini hakikutekeleza maagizo hayo hivyo Baraza limechukua hatua ya kukifungia kiwanda hicho mpaka kitakapo tekeleza maelekezo yote yaliyotolewa na NEMC.
Ameongeza kuwa NEMC inaunga mkono uwekezaji nchini kwa kuwataka wawekezaji wote kufuata taratibu zote za Kimazingira zinazotolewa na NEMC zikiwemo kufanya Tathmini ya Athari kwa Mazingira na kupatiwa cheti Cha Mazingira.
Kwa upande wake, Kaimu Meneja wa Kanda ya Mashariki Kusini (NEMC) Bw. Noel Kikwale amezitaka Mamlaka zinazohisika na Mipango miji kutenga Maeneo maalumu ya viwanda na kuhakikisha wawekezaji wanafanya shughuli zao katika Maeneo hayo ili kuepuka changamoto za kimazingira na afya ya wananchi.
Ukaguzi huo ulihusisha wataalamu wa Mazingira kutoka NEMC wakiongozwa na Meneja wa Utekelezaji wa Sheria Mhandisi Bi. Luvilo Mwamila na Viongozi wa Kata ya Vikindu na wa Serikali za mitaa.



from MALUNDE 1 BLOG https://ift.tt/ZVwxt4Y








No comments