TAASISI YA DORIS MOLLEL YAOKOA WATOTO NJITI KWIMBA,Jengo la kisasa laanza kazi

-Doris Mollel Foundation (DMF) yajenga jengo la kisasa la kimataifa lenye thamani ya Sh. bilioni 2.125 kuhudumia watoto wanaozaliwa kabla ya wakati (njiti).
-Wananchi wa Kwimba waishukuru taasisi hiyo kwa kusogeza huduma karibu; wasema awali walisafiri umbali mrefu kufuata matibabu.
- Shirika la Afya Duniani (WHO) lasema mradi huo unaendana na miongozo ya kimataifa ya kuhakikisha mama na mtoto wanabaki pamoja wakati wa matibabu.
Wananchi Wilayani Kwimba na maeneo jirani wameishukuru Doris Mollel Foundation kwa kuleta mabadiliko makubwa katika Wilaya ya Kwimba, Mwanza, baada ya kufadhili na kusimamia ujenzi wa jengo la kisasa la kimataifa la kuwahudumia watoto wanaozaliwa kabla ya wakati (njiti) katika Hospitali ya Wilaya ya Kwimba. Jengo hilo linasogeza huduma hizi muhimu karibu na wananchi kwa mara ya kwanza.
Mkuu wa Wilaya ya Kwimba, Mhe. Ng’wilabuzu Ludigija, ameridhishwa na utekelezaji wa mradi huo unaofadhiliwa na Taasisi ya Doris Mollel, akieleza kuwa jengo hilo litakuwa na mchango mkubwa katika kuokoa maisha ya watoto wachanga.
Mkazi wa Kwimba, Joyce Emmanuel James, ameishukuru Taasisi ya Doris Mollel Foundation kwa kujenga jengo hilo, akieleza changamoto walizokuwa wanapitia kabla ya uwepo wa huduma hizo karibu na jamii, ikiwemo kulazimika kusafiri umbali mrefu kufuata matibabu.
Kwa upande wake, Mwakilishi wa World Health Organization (WHO) nchini Tanzania, Dkt. Alex Ntale Gasasira, ametambua uwekezaji huo na kusisitiza umuhimu wa uwepo wa huduma hizi karibu na jamii. Ameeleza kuwa mfumo huo unaendana na miongozo ya WHO inayosisitiza umuhimu wa mama na mtoto kuwa pamoja wakati wa matibabu ili kuongeza nafasi ya mtoto kuishi.
Jengo hilo la kimataifa linalotarajiwa kuzinduliwa tarehe 28 Februari 2026 limefadhiliwa na kujengwa na Doris Mollel Foundation (DMF) kwa lengo la kuboresha huduma za watoto wachanga na kuleta matumaini mapya kwa familia za Kwimba na maeneo ya jirani. Mradi huo umegharimu takribani Shilingi bilioni 2.125 kwa kushirikiana na Keep a Child Alive na Jhpiego







No comments