WANACHAMA WA CCM KATA YA NYAMALOGO WAADHIMISHA MIAKA 49 KWA KUPANDA MITI, VIJANA WAHIMIZWA KUCHANGAMKIA FURSA ZA UONGOZI
Na Michael Abel
Wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Kata ya Nyamalogo, Wilaya ya Shinyanga Vijijini, wameadhimisha miaka 49 ya kuzaliwa kwa chama hicho kwa kufanya shughuli ya upandaji miti, ikiwa ni sehemu ya kuhamasisha uhifadhi wa mazingira na mshikamano miongoni mwa wanachama.
Maadhimisho hayo yamefanyika leo Februari 8, 2026 katika kata ya Nyamalogo halmashauri ya Shinyanga Mkoani Shinyanga, yaliyotanguliwa na zoezi la upandaji miti kwa wanachama wa Chama cha Mapinduzi.
Akizungumza katika maadhimisho hayo, Katibu wa CCM Wilaya ya Shinyanga Vijijini, Bi. Erenestina Richard, amewahimiza vijana wa chama hicho kuchangamkia fursa za uongozi zilizopo ndani ya CCM kuanzia ngazi ya balozi, akisema vijana wana nafasi kubwa ya kuendeleza misingi na dira ya chama iwapo watashiriki kikamilifu katika uongozi.
Bi. Erenestina ameongeza kuwa CCM inaendelea kuwa shule ya uongozi kwa vijana, na kwamba chama kinaamini katika kuwajenga viongozi kuanzia ngazi za chini ili kuandaa kizazi chenye maadili, uzalendo na uwezo wa kuwatumikia wananchi kwa ufanisi.
Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Nyamalogo Mhe. Titus Kalemela amesema maadhimisho ya miaka 49 ya CCM ni fursa ya kutafakari safari ya chama tangu kuanzishwa kwake na kuwataka wanachama kuendeleza umoja, mshikamano na kufanya kazi kwa bidii ili kukiendeleza chama na kuwatumikia wananchi wa kata hiyo.
Katika hotuba yake ya shukrani, Mhe. Kalemela amewapongeza wazee na waasisi wa chama kwa mchango wao mkubwa uliokifanya CCM kufika ilipo leo, akisisitiza kuwa ni wajibu wa kizazi cha sasa kuendeleza misingi waliyoiacha kwa vitendo, ikiwemo kulinda mazingira na kushiriki kikamilifu katika shughuli za chama.
<<<TAZAMA PICHA MATUKIO MBALIMBALI>>>

Katibu wa CCM Wilaya ya Shinyanga Vijijini, Bi. Erenestina Richard akipanda mti kwenye maadhimisho hayo.
Diwani wa Kata ya Nyamalogo Mhe. Titus Kalemela akizungumza kwenye maadhimisho hayo.

Katibu wa CCM Wilaya ya Shinyanga Vijijini, Bi. Erenestina Richard akizungumza kwenye maadhimisho hayo.
from MALUNDE 1 BLOG https://ift.tt/XyGhzN0













































No comments