Breaking News

KISHAPU YAZINDUA CHANJO YA POLIO, WATOTO 120, 000 KUFIKIWA

Na Sumai Salum – Kishapu

Katika hatua muhimu ya kuimarisha afya ya jamii, Wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga imezindua rasmi kampeni ya chanjo ya ugonjwa wa Polio, ikiwa ni sehemu ya jitihada za serikali kuhakikisha watoto wanalindwa dhidi ya ugonjwa huo hatari.


Uzinduzi wa kampeni hiyo umefanyika Machi 24, 2026 katika Shule ya Msingi Buduhe, iliyopo Kata ya Kishapu, ambapo wananchi, viongozi wa serikali na wataalamu wa afya walihudhuria na kusisitiza umuhimu wa zoezi hilo kwa ustawi wa jamii.


Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya, Fadhili Mvanga amesema kuwa kuanzishwa kwa kampeni hiyo kunatokana na uwepo wa viashiria vya vimelea vya ugonjwa wa polio vilivyobainika katika maji taka mkoani Mwanza hivyo kuilazimu serikali kuja na mpango wa kukinga watoto katika mikoa saba hali inayohitaji tahadhari ya haraka ili kuzuia kusambaa kwa ugonjwa huo.


Ameeleza kuwa lengo kuu la serikali ni kulinda afya za wananchi, hususan watoto, kwa kuhakikisha wanapatiwa chanjo kwa wakati. Amebainisha kuwa kampeni hiyo itafanyika kwa siku nne mfululizo, ikiwalenga watoto wenye umri chini ya miaka 10 kupitia vituo vya afya elekezi, majumbani na mashuleni.


“Serikali imeweka kipaumbele katika ustawi endelevu wa afya za wananchi. Ndiyo maana inaendelea kuboresha miundombinu ya sekta ya afya kupitia Wizara ya Afya, na huduma hii ya chanjo inatolewa bure kwa wote,” amesema Mvanga.


Aidha, ametoa wito kwa wakazi wa Kishapu kujitokeza kwa wingi kushiriki kampeni hiyo, huku akisisitiza kuwa hakuna kiongozi wala mwananchi anayepaswa kukwamisha zoezi hilo muhimu kwa mustakabali wa afya ya jamii.


Kwa upande wake, Mratibu wa chanjo wilayani humo, Jamila Mohamed, amesema jumla ya watoto 120,000 wanatarajiwa kufikiwa katika kampeni hiyo. Amefafanua kuwa chanjo ya polio ni muhimu sana kwani husaidia kuzuia madhara makubwa ikiwemo kupooza kwa misuli na kupelekea ulemavu wa kudumu na hata vifo.


Naye mwananchi wa Mtaa wa Mwasele ‘B’, Rodah Zacharia, ameipongeza serikali kwa juhudi zake za kuimarisha sekta ya afya. Amesema maboresho ya huduma za afya yameongeza upatikanaji wa huduma kwa urahisi na kwa wakati, huku akiwahimiza wazazi na walezi kujitokeza kwa wingi kuhakikisha watoto wao wanapata chanjo.

Kampeni hiyo ni sehemu ya mkakati mpana wa serikali wa kutokomeza kabisa ugonjwa wa polio nchini, na inatarajiwa kuwa na mchango mkubwa katika kulinda kizazi cha sasa na kijacho.Mwakilishi wa Mkuu wa Wilaya ya Kishapu mkani Shinyanga ambaye pia ndie mgeni rasmi, Fadhili Mvanga (Afisa tawala wilayani humo) akizungumza wakati wa uzinduzi wa kampeni ya chanjo ya Polio ngazi ya Wilaya uliofanyika katika Shule ya Msingi Buduhe Kata ya Kishapu Machi 24,2026Mwakilishi wa Mganga mkuu wa Wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga Jofrey George Shinyangwe akizungumza kwenye uzinduzi wa kampeni ya chanjo ya polio ngazi ya wailaya Machi 24,2026 walipokuwa Shule ya msingi Buduhe
Mwakilishi wa Mkuu wa Divisheni ya Elimu ya Awali na Msingi Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga ambaye pia ni Afisa Elimu ya Watu Wazima na Nje ya Mfumo Rasmi Mwl. Baraka Mwijarubi akizungumza kwenye uzinduzi wa kampeni ya chanjo ya polio ngazi ya wailaya Machi 24,2026 walipokuwa shule ya msingi Buduhe
Afisa tarafa ya Kishapu wilayani Kishapu mkoani Shinyanga, Tano Malele akizungumza wakati wa uzinduzi wa kampeni ya chanjo ya Polio ngazi ya Wilaya uliofanyika katika Shule ya Msingi Buduhe Kata ya Kishapu Machi 24,2026
Mratibu wa chanjo Wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga, Jamila Mohamed, akieleza mikakati ya kufikia zaidi ya watoto 120,000 kupitia kampeni ya chanjo ya polio inayoendelea wilayani humo akizungumza wakati wa uzinduzi Machi 24, 2026 katika viwanja vya Shule ya msigi Buduhe
Mratibu wa afya kwa umma wilayani Kishapu mkoani Shinyanga, Mwajuma Abeid akifurahia mkutano wa uzinduzi kampeni ya chanjo ya poli ngazi ya wilaya Machi 24, 2026 viwanja vya Shule ya msingi Buduhe.

Mkaazi wa Mtaa wa Mwasele ‘B’, Kata ya Kishapu wilayani Kishapu mkoani Shinyanga Rodah Zacharia, akitoa maoni yake kuhusu kampeni ya chanjo ya polio iliyozinduliwa kiwilaya viwanja vya Shule ya msingi buduhe wilayani humo Machi 24, 2026 baada ya watoto wake kupata chanjo hiyo mapema























































from MALUNDE 1 BLOG https://ift.tt/SAZ3vIV

No comments