Breaking News

NCAA YACHUKUA HATUA KULINDA MIMEA TIBA NGORONGORO, ZAIDI YA AINA 30 YATAJWA

 

Na Bora Mustafa, Arusha.

Kutokana na ongezeko la wananchi kuvamia hifadhi kwa lengo la kutafuta mimea tiba, Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) imechukua hatua mahsusi kuhakikisha upatikanaji endelevu wa mimea hiyo bila kuathiri uhifadhi wa mazingira.

Akizungumza kuelekea kilele cha maadhimisho ya Wiki ya Wanyamapori Duniani jijini Arusha, Afisa Misitu wa Idara ya Ikolojia wa NCAA, Naamani N. Namani, amesema kuwa zaidi ya aina 30 za mimea tiba zimeainishwa ndani ya eneo la hifadhi hiyo.

Amesema mimea hiyo imekuwa ikitumika kwa muda mrefu na makabila ya asili kama Wahadzabe, Wadatoga na Wamasai kwa matibabu ya jadi, wakitumia maarifa ya asili bila kuhatarisha wanyamapori wala mazingira ya hifadhi.

Aidha, Namani amesema ili kupunguza shinikizo la wananchi kuvamia hifadhi, mamlaka imeanzisha vitalu vya miti nje ya eneo lililohifadhiwa. Kupitia mpango huo, zaidi ya miche laki moja hupandwa kila mwaka.

Ameeleza kuwa hatua hiyo inalenga kuhakikisha mimea tiba inakuwa rasilimali endelevu, huku ikilinda  na kuhakikisha vizazi vya sasa na vijavyo vinanufaika.

Namani amesisitiza kuwa dawa za asili si tiba pekee bali ni sehemu ya urithi wa kitamaduni unaopaswa kulindwa na kuendelezwa kwa manufaa ya jamii na mazingira kwa ujumla.



from MALUNDE 1 BLOG https://ift.tt/qvZOw6h

No comments