SERIKALI KUENDELEA KUBORESHA VITUO VYA MAARIFA NCHINI.



Na, Mwandishi wetu - Pwani

SERIKALI kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu) imeeleza dhamira yake ya kuendelea kuboresha Vituo vya Maarifa nchini, hususan vile vinavyotoa huduma kwa madereva wa malori ya masafa marefu kuhusu masuala ya VVU na UKIMWI.

Kauli hiyo imetolewa na Katibu Mkuu wa Ofisi hiyo, Dkt. Jim Yonazi mapema mwanzoni mwa wiki mara baada ya kutembelea na kukagua Vituo vya Maarifa vinavyotoa huduma za VVU na UKIMWI kwa madereva wa malori ya masafa marefu vilivyopo eneo la Kurasini katika wilaya ya Temeke Jijini Dar es Salaam na Mdaula mkoa wa Pwani ambayo Vituo hivyo vipo chini ya Tume ya Kudhibiti UKIMWI Tanzania (TACAIDS).

Dkt. Yonazi amesema Serikali, kupitia Tume ya Kudhibiti UKIMWI Tanzania (TACAIDS), ina jukumu la kusogeza huduma muhimu za VVU na UKIMWI karibu na wananchi.

“Vituo hivi vina mchango mkubwa katika kuwafikia madereva wa masafa marefu ambao mara nyingi hukaa safarini kwa muda mrefu. Serikali itaendelea kuviboresha hususan kwenye miundombinu ya kutolea huduma na kuongeza wataalam wa afya ili viweze kutoa huduma bora Kwa madereva hao wa masafa marefu kwa kujua afya zao dhidi ya maambukizi ya virusi vya UKIMWI,” amesema Dkt. Yonazi.

Kwa upande wao, madereva wa malori ya masafa marefu wanaonufaika na huduma hizo wameeleza kuwa Vituo vya Maarifa ni msaada mkubwa kwao, kwani vinawapa fursa ya kupata elimu na huduma za VVU na UKIMWI kwa urahisi na bila gharama na kuipongeza Serikali kwa namna inavyoendelea kujali na kuwafikia wananchi wake.










from MALUNDE 1 BLOG https://ift.tt/YMkbA0Z

Post a Comment

Previous Post Next Post