Breaking News

TMC kuileta Afrika pamoja kujadili mustakabali wa kidijitali,wadau zaidi ya 200 kushiriki

Na Mwandishi wetu, Dar es Salaam

Zaidi ya watu 200 wanatarajiwa kushiriki Jukwaa la Afrika la Ubunifu na Teknolojia 2026 litakalofanyika Juni 16 na 17 mwaka huu jijini Dar es Salaam, likiwakutanisha wadau mbalimbali kujadili mustakabali wa kidijitali nchini.

Jukwaa hilo ambalo limeandaliwa na Taasisi ya Tech & Media Convergency (TMC) na linatarajiwa kuwakutanisha viongozi wa serikali, wadhibiti, sekta binafsi, wabunifu, wasomi, asasi za kiraia zinazofanyakazi kwenye masuala ya ubunifu na teknolojia pamoja na wataalamu wa kiufundi.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Mwanzilishi na Mkurugenzi Mtendaji wa TMC, Asha Abinallah amesema jukwaa hilo linafanyika kwa kushirikiana na Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari na litahudhuriwa pia na washirika wa maendeleo pamoja na jumuiya ya kimataifa ya sera za kidijitali.



Amesema jukwaa hilo la mwaka huu linabeba kauli mbiu ya “Kuongoza mustakabali wa kidijitali: Kuunganisha usimamizi wa mtandao, data, usalama wa mtandao na sera za kimkakati za teknolojia.”

Abinallah amesema kuwa jukwaa la mwaka huu linapanua wigo wake kutoka ngazi ya kitaifa hadi bara la Afrika, likiunganishwa na programu ya Tanzania Digital Collaboration (TDC) kwa lengo la kuimarisha usimamizi wa kidijitali unaojumuisha wadau wote.

Amesema jukwaa hilo linamalengo ya kuimarisha ushiriki jumuishi wa wadau mbalimbali katika michakato ya usimamizi wa kidijitali, kuoanisha mifumo ya sera katika usimamizi wa mtandao data na usalama mtandao.

“Malengo mengine ya jukwaa ni kuzalisha mapendekezo ya sera yanayotekelezeka na yanayotegemea ushahidi ili kuongoza mikakati ya kitaifa ya Tehama na mageuzi ya kisheria pamoja na kuimarisha utekelezaji wa ulinzi wa data na uimara wa usalama wa mtandao,” amesema Abinallah 

Amesisitiza kuwa jukwaa hilo litajumuisha mijadala ya ngazi ya juu, majadiliano ya sera na uzinduzi wa tafiti muhimu, sambamba na kuwezesha ushirikiano kati ya watunga sera, wabunifu chipukizi (startups), wawekezaji, wataalamu na wananchi kwa ujumla.

“Matokeo yanayotarajiwa kupitia jukwaa hilo ni pamoja na kuimarika kwa uratibu wa taasisi, kuwepo kwa mazingira bora na yanayotabirika kwa uwekezaji wa kidijitali, ulinzi imara wa haki za kidijitali pamoja na kuongezeka kwa ushirikiano kati ya wadau wa Tanzania na wa kimataifa,” amesema Abinallah

Aidha Abinallah amesema tangu mwaka 2021 taasisi hiyo imekuwa ikiandaa jukwaa la ubunifu na teknolojia nchini Tanzania, ambalo limejijengea sifa kama jukwaa la kitaifa linaloaminika katika kuendeleza mijadala kuhusu mabadiliko ya kidijitali, mageuzi ya kisheria, haki za kidijitali na uimara wa usalama wa mtandao.

Kwa mujibu wa Abinallah, uchumi wa kidijitali barani Africa unaendelea kukua kwa kasi, huku makadirio yakionesha mchango wake kufikia dola za Marekani bilioni 180 kwa mwaka 2025 na bilioni 712 ifikapo mwaka 2050.

Hata hivyo, amesema ukuaji huo unaambatana na changamoto za kimuundo ikiwemo mifumo iliyogawanyika ya usimamizi, kiwango cha chini cha upatikanaji wa intaneti, kuzimwa kwa huduma za intaneti, kufungwa kwa majukwaa ya kidijitali pamoja na ongezeko la vitisho vya usalama wa mtandao.

No comments