MIGODI YA BARRICK YA BULYANHULU NA NORTH MARA YAADHIMISHA SIKU YA MAZINGIRA KWA KUPANDA MITI NA KUFUATILIA MRADI WA UREJESHAJI UOTO ASILI MTO TIGHITE

Wafanyakazi wa Barrick Bulyanhulu wakiwa kwenye picha ya pamoja na wanafunzi baada ya kushiriki zoezi la upandaji wa miti kwenye maadhimisho ya siku ya mazingira duniani.
Afisa Mahusiano ya Jamii Mwandamizi wa Mgodi wa Barrick Bulyanhulu , Zuwena Senkondo akimwagilia mti baada ya upandaji katika maadhimisho ya siku ya mazingira duniani
Wafanyakazi wa Barrick North Mara wakipanda miti kando kando ya Mto Tighite katika maadhimisho ya siku ya mazingira duniani Wilayani Tarime , Mkoani Mara.
***

Kampuni ya Barrick inayoendesha shughuli zake nchini kwa ubia na Serikali kupitia kampuni ya Twiga, kupitia migodi yake ya Bulyanhulu na North Mara imeadhimisha Siku ya Mazingira Dunia 2026 kwa kushirikiana na jamii zinazoizunguka kwa kupanda miti, kufanya usafi kwenye shule na kukagua maendeleo ya mradi wa kurejesha uoto wa asili wa Mto Tighite uliopo wilayani Tarime.

Mgodi wa Barrick Bulyanhulu ulipo katika Halmashauri ya wilaya ya Msalala mkoani Shinyanga wafanyakazi wake walitembelea Shule ya Msingi Kakola A na kupanda miti pamoja na kufanya usafi pia ulitoa msaada wa miche ya miti ya matunda na kivuli ipatayo 2300.

Kwa upande wa Mgodi wa Barrick North Mara uliopo wilayani Tarime mkoani Mara, Wafanyakazi wake waliungana na jamii kutembelea na kukagua maendeleo ya mradi wa kurejesha uoto wa asili wa mto Tighite uliopo katika Kijiji cha Matongo unaofadhiliwa na mgodi huo kupitia shirika lisilo la Kiserikali la Jumuiya ya Watumiaji Maji Tighite Chini (JWMTC).

Kaimu Meneja Mazingira wa Barrick Bulyanhulu, Arespicius Onesmo akizungumzia kuhusu ushiriki wa Barrick Bulyanhulu katika maadhimisho ya mwaka huu,alisema ni mwendelezo wa utekelezaji wa mkakati wa kampuni ambapo suala la mazingira linapewa kipaumbele kikubwa.

“Tumeshirikiana na jamii kuadhimisha Siku ya Mazingira Duniani kwa kupanda miti, tumeanzia ndani ya mgodi ambapo wafanyakazi wa kila idara wameshirikiana na viongozi wao kupanda miti, na hii inaonesha uwajibikaji wa mgodi katika kulinda na kutunza mazingira vilevile mgodi una programu ya kutoa miche zaidi ya 20,000 katika shule zilizopo katika kata mbili za Bugarama na Bulyanhulu ili kuboresha mazingira”,alisema Onesmo.

Naye Meneja Mazingira wa Barrick North Mara, Frank Ngoloma alisema maadhimisho ya mwaka huu wameyafanya kwa kufuatilia maendeleo ya ukuaji wa miti ya asili iliyopandwa kandokando ya mto Tighite kwa ufadhili wa mgodi na wameridhishwa na usimamizi mzuri wa mradi huo na miti iliyopandwa mwaka jana inaendelea kustawi vizuri

Ngoloma alisema mradi huo ulizinduliwa wakati wa maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani mwaka jana kwa lengo la kurejesha uoto wa asili wa mto huo unaotegemewa na maelfu ya wananchi kwa ajili ya maji ya matumizi ya majumbani,kunywesha mifugo na shughuli za kilimo.

Akizungumzia ushiriki wa Barrick kushirikiana na jamii kuadhimisha Siku ya Mazingira Duniani kila mwaka, kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Msalala , Humphrey Peter aliupongeza Mgodi wa Bulyanhulu kwa kuthamini maadhimisho hayo na kuona umuhimu wa kushirikiana na jamii katika zoezi la kupanda miti ili kulinda mazingira.

“Tunaushukuru Mgodi wa Barrick Bulyanhulu kwa kutambua siku ya mazingira dunia, kati ya taasisi na mashirika yaliyopo katika wilaya yetu ni Barrick Bulyanhulu pekee ndio wanafanya tukio hili la kipekee na wanakuja kusaidiana na jamii kuboresha Mazingira ,” amesema Humphrey.

Naye Mwenyekiti wa JWMTC, Mwita Seri na Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Matongo,Charles Ryoba wameushukuru mgodi wa Barrick North Mara kwa ufadhili na ushirikiano unaoendelea kutoa kwa ajili ya utekelezaji wa mradi wa kuboresha mazingira ya mto Tighite unaolenga kufanikisha upandaji wa miti ya asili 50,000 .

Kwa mujibu wa taarifa iliyosomwa, JWMTC iliomba Mgodi wa Barrick North Mara ukakubali kutoa shilingi milioni 36.7 kwa ajili ya kuotesha miche kwenye vitalu, kisha kupanda miti ya asili 50,000 katika eneo lenye ukubwa wa hekta 27 kandokando ya Mto Tighite.

Aidha, Mto Tighite ni miongoni mwa vyanzo muhimu vinavyochangia maji katika Mto Mara ambao unamwaga maji yake katika la ziwa la kimataifa - Ziwa Victoria upande wa Tanzania.

Kampuni ya Barrick katika mikakati yake endelevu moja ya sera katika uendeshaji shughuli zake mambo ya mazingira na mabadiliko ya tabianchi yanapewa vipaumbele katika utunzaji wa mazingira , kulinda vyanzo ya maji, uchafunzi wa hali ya hewa na kulinda uoto wa asili.
Wafanyakazi wa Barrick Bulyanhulu wakiwa kwenye picha ya pamoja na wanafunzi na wadau wengine mara baada ya zoezi la upandaji wa miti katika maadhimisho ya siku ya mazingira duniani
Wafanyakazi North Mara wakiongea na wananchi baada ya kutembelea mto Tighite
Wafanyakazi North Mara wakiongea na wananchi baada ya kutembelea mto Tighite



from MALUNDE 1 BLOG https://ift.tt/RebomuE

Post a Comment

Previous Post Next Post