TGNP YATAKA NGUVU ZAIDI KATIKA UTEKELEZAJI WA BAJETI YA 2026/2027

Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP) umeiomba Serikali kuhakikisha Bajeti ya Mwaka wa Fedha 2026/2027 inatekelezwa kwa ufanisi ili kufanikisha malengo ya maendeleo ya taifa yaliyowekwa katika Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

Akizungumza jijini Dar es Salaam wakati wa mjadala na uchambuzi wa Bajeti ya Taifa ya mwaka 2026/2027 kupitia jukwaa la Kijiwe cha Kahawa, mwakilishi wa TGNP, Flora Ndaba, alisema pamoja na bajeti ya mwaka huu kuonesha kuzingatia masuala ya usawa wa kijinsia, bado kuna umuhimu wa kuweka nguvu kubwa katika utekelezaji wake ili matokeo yaliyokusudiwa yaweze kupatikana.
Alisema utekelezaji madhubuti wa bajeti ndiyo utakaowezesha wananchi, hususan wanawake, vijana na makundi yaliyo pembezoni, kunufaika na rasilimali zilizotengwa na serikali.

Kwa upande wake, Evans Exaud alisema bajeti ya mwaka huu imeonesha kuipa kipaumbele sekta binafsi, hususan wafanyabiashara, jambo ambalo linaweza kuchochea ukuaji wa uchumi na kuongeza fursa za ajira kwa wananchi.
Alieleza kuwa mazingira bora ya biashara yatasaidia kufikia malengo ya maendeleo yaliyowekwa na serikali kwa kuongeza uzalishaji na mapato ya taifa.

Wakati huo huo, baadhi ya vijana waliohudhuria mjadala huo walitoa maoni tofauti kuhusu bajeti hiyo, wakisisitiza umuhimu wa serikali kuendelea kuangalia hali halisi ya maisha ya wananchi ili kuhakikisha maendeleo yanayopatikana yanawanufaisha wote.

Awali, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TGNP, Clara Kalanga, alisema jukwaa hilo linalenga kutathmini Bajeti ya Taifa ya mwaka 2026/2027 kwa mtazamo wa kijinsia na kuangalia namna itakavyowezesha kufikiwa kwa malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

Kalanga alisema bajeti yenye kuzingatia usawa wa kijinsia ni nyenzo muhimu katika kuhakikisha makundi yote ya jamii yanashiriki na kunufaika na maendeleo ya taifa kwa usawa.
Wadau wa maendeleo, wanaharakati, wataalamu wa uchumi na viongozi wa serikali za mitaa wakifuatilia mjadala wa uchambuzi wa Bajeti ya Taifa ulioandaliwa na Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP) kupitia jukwaa la Kijiwe cha Kahawa.


from MALUNDE 1 BLOG https://ift.tt/D2TLHKs

Post a Comment

Previous Post Next Post