Na Dotto Kwilasa, Dodoma
Serikali imesema itaendelea kuwekeza kwa kiwango kikubwa katika sekta za elimu, mawasiliano na huduma za kijamii mkoani Dodoma, huku ikiahidi kuondoa changamoto za mawasiliano na kuimarisha miundombinu ya maendeleo ifikapo mwaka 2030.
Hayo yameelezwa Julai 23, 2026 na Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Angellah Jasmine Mbelwa Kairuki, wakati wa ziara yake ya kikazi Wilaya ya Mpwapwa iliyolenga kukagua miradi ya maendeleo na kusikiliza kero za wananchi katika Kijiji cha Mlembule.
Akizungumza na wananchi Wilayani humo, Waziri Kairuki amesema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imeendelea kutekeleza kwa vitendo Ilani ya CCM ya mwaka 2025–2030 kwa kuwekeza katika miradi inayogusa maisha ya wananchi, hususan elimu, afya, mawasiliano, maji na miundombinu.
Katika sekta ya elimu, amesema ndani ya kipindi cha miaka mitano Serikali imejenga shule mpya 12 katika Wilaya ya Mpwapwa kwa gharama ya shilingi bilioni 15.1. Aidha, madarasa 251, mabweni 11, matundu ya vyoo 265, maabara tano za sayansi, nyumba saba za walimu na mabwalo manne ya chakula kwa wanafunzi yamejengwa ili kuboresha mazingira ya kujifunzia.
Ameongeza kuwa katika mwaka wa fedha 2026/27, Serikali imetenga shilingi milioni 562.9 kwa ajili ya ujenzi wa shule mpya ya sekondari pamoja na matundu ya vyoo, hatua inayolenga kuongeza fursa za elimu kwa watoto wa Mpwapwa.
Mbali na elimu, Waziri Kairuki amesema Serikali imepiga hatua kubwa katika sekta ya mawasiliano ambapo mkoani Dodoma tayari minara 488 ya mawasiliano imesimikwa, huku zaidi ya wananchi 150,000 wakinufaika na huduma bora za mawasiliano na matumizi ya mkongo wa taifa wa mawasiliano wenye urefu wa kilomita 942.5.
Amesema Serikali inaendelea na utekelezaji wa miradi ya kimkakati ya mawasiliano, ikiwemo kukamilisha minara 636 ifikapo Machi 2027 pamoja na mradi mwingine wa minara 280, sambamba na kufanya tathmini ya maeneo yenye changamoto ili kuhakikisha huduma za mawasiliano zinawafikia wananchi wote.
Kairuki amesisitiza kuwa uboreshaji wa miundombinu ya TEHAMA ni sehemu ya mkakati wa Serikali wa kujenga uchumi wa kidijitali na kuongeza fursa za elimu, biashara na utoaji wa huduma za Serikali kwa njia ya mtandao.
Katika ziara hiyo, Waziri huyo pia aliweka jiwe la msingi la shule mpya ya msingi na awali katika Kijiji cha Mlembule pamoja na kukagua ujenzi wa chumba maalumu cha TEHAMA, ambapo alitangaza kuwa Serikali itapeleka kompyuta 22 kwa ajili ya kuwawezesha wanafunzi kujifunza kwa kutumia teknolojia.
Kwa upande wake, Mbunge wa Jimbo la Mpwapwa, Adam Malima, amesema pamoja na hatua kubwa iliyofikiwa katika ujenzi wa minara ya mawasiliano, bado yapo maeneo yanayokumbwa na changamoto ya mtandao, ikiwemo Kijiji cha Mlembule ambako wananchi hutegemea mawasiliano kutoka minara ya maeneo jirani.
Ameiomba Serikali kuharakisha utekelezaji wa miradi ya mawasiliano ili kuhakikisha wananchi wa maeneo yote ya jimbo hilo wanapata huduma bora za mawasiliano.
from MALUNDE 1 BLOG https://ift.tt/2Yjk4xa
Tags
News



