Na Dotto Kwilasa,Dodoma
Uwekezaji mkubwa unaofanywa na Serikali katika sekta za afya, elimu, maji, nishati na miundombinu umeendelea kubadili sura ya Wilaya ya Kongwa mkoani Dodoma,huku Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Angellah Jasmine Mbelwa Kairuki akisema hatua hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa maelekezo ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuhakikisha maendeleo yanawafikia wananchi moja kwa moja.
Waziri Kairuki amesema Serikali imeendelea kupeleka fedha nyingi kwenye miradi mbalimbali ya maendeleo, hivyo sasa ni wajibu wa watendaji kuhakikisha uwekezaji huo unazalisha matokeo yanayoonekana katika maisha ya wananchi.
Waziri ameeleza hayo leo Julai 24,2026 katika Kijiji cha Laikala, Kata ya Sagara, Wilaya ya Kongwa, wakati akiweka jiwe la msingi la ujenzi wa Kituo cha Afya Laikala, ikiwa ni ziara yake ya kukagua utekelezaji wa miradi ya maendeleo mkoani Dodoma Kwa lengo la kujionea utekelezaji wa miradi, kubaini changamoto zilizopo na kuchochea kasi ya maendeleo.
"Serikali imepeleka fedha nyingi kwenye miradi ya maendeleo,tunajivunia vituo vya afya, shule, miradi ya maji na miundombinu mingine sasa tunataka kuona fedha hizo zinabadilisha maisha ya wananchi kupitia huduma bora na miradi yenye tija," amesema Kairuki.
Amebainisha kuwa katika mwaka wa fedha uliopita, Wilaya ya Kongwa ilipokea zaidi ya Sh bilioni 8.6 kwa ajili ya kutekeleza miradi katika sekta za afya, elimu, maji, kilimo, umwagiliaji na mifugo.
Amesema maendeleo ya Kongwa hayawezi kujengwa na Serikali pekee, bali yanahitaji ushiriki wa wananchi kwa kutumia ipasavyo fursa zilizopo katika kilimo, mifugo na sekta nyingine za uzalishaji.
"Kongwa itajengwa na wana Kongwa wenyewe,kila mmoja atimize wajibu wake,fedha mnazochangia kupitia kodi na ushuru lazima muone matokeo yake kupitia huduma bora na miradi yenye ufanisi," amesema.
Kwa upande wa sekta ya afya, Kairuki amemuelekeza Mganga Mkuu wa Kituo cha Afya Laikala kuhakikisha anafuatilia kwa karibu utoaji wa huduma ili wananchi wanufaike na uwekezaji unaofanywa na Serikali.
Aidha, amewataka watumishi wa afya nchini kuzingatia viapo vyao vya kazi kwa kutoa huduma kwa kufuata maadili ya taaluma, utu na heshima kwa wananchi.
Amesema Serikali imeendelea kuboresha huduma za afya Kongwa ambapo wilaya hiyo sasa ina vituo vya afya 11, magari saba ya wagonjwa pamoja na nyumba za watumishi.
Pia amewahimiza wananchi kujiunga na Mpango wa Bima ya Afya kwa Wote ili kuwawezesha kupata matibabu kwa urahisi wanapokumbwa na changamoto za kiafya.
Akizungumzia elimu, Kairuki amesema Serikali itaendelea kuhakikisha kila mtoto mwenye umri wa kwenda shule anapata elimu bila vikwazo.
Amesema katika Wilaya ya Kongwa, Serikali imeelekeza zaidi ya Sh bilioni 1.2 kwa elimu ya msingi na Sh bilioni 1.4 kwa elimu ya sekondari kupitia mpango wa elimu bila ada.
Ameongeza kuwa zaidi ya madarasa 670 yamejengwa, hatua iliyosaidia kupunguza umbali wa wanafunzi kufuata shule na kuongeza mazingira bora ya kujifunzia.
"Hakuna kisingizio tena kwa mtoto kushindwa kupata elimu Serikali itaendelea kujenga shule za kutosha kuhakikisha watoto wote wanapata haki hiyo," amesema.
Katika huduma ya maji, Kairuki amesema Serikali inatambua changamoto iliyopo katika baadhi ya maeneo ya Kongwa na imeanza hatua za kuchimba visima 19 ili kuongeza upatikanaji wa maji safi na salama.
Kwa upande wa kilimo na mifugo, amesema Serikali itaendelea kuwawezesha wananchi kupitia upatikanaji wa mbolea, pembejeo bora, dawa za mifugo, huduma za ugani pamoja na vitendea kazi kwa maafisa ugani na mifugo.
"Lengo ni kuongeza uzalishaji, kuinua kipato cha wakulima na wafugaji na kujenga uchumi wa wananchi,"amesisitiza
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Kongwa, Simon Mayeka, amesema wilaya hiyo imepiga hatua kubwa katika sekta za afya na elimu kutokana na uwekezaji unaofanywa na Serikali.
Amesema wakati Rais Samia Suluhu Hassan anaingia madarakani, Kongwa ilikuwa na vituo vinne vya afya lakini sasa imefikia 11 baada ya Serikali kujenga vituo saba vipya.
Amesema hatua hiyo imesaidia kupunguza vifo vya mama na mtoto kutokana na kuboreshwa kwa huduma za afya.
Amesema Kwa upande wa nishati kata zote 22 za Kongwa zimefikiwa na umeme na sasa wananchi wanapaswa kutumia fursa hiyo kuongeza shughuli za uzalishaji.
from MALUNDE 1 BLOG https://ift.tt/mcxpria
Tags
News





