Ndejembi: Serikali kuimarisha usafirishaji n usambazaji wa umeme nchini.



Waziri wa Nishati, Deogratius Ndejembi, amesema Serikali inaendelea kuimarisha miundombinu ya usafirishaji na usambazaji wa umeme nchini ili kuhakikisha ongezeko la uzalishaji linaendana na upatikanaji wa umeme wa uhakika kwa wananchi na shughuli za kiuchumi, akisisitiza kuwa hatua hiyo ni sehemu ya kutekeleza maelekezo na maono ya Rais Samia Suluhu Hassan.

Akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa Mradi wa Kufua Umeme wa Bwawa la Mwalimu Nyerere mkoani Pwani, Ndejembi amesema Serikali imekamilisha kwa asilimia 98 ujenzi wa njia ya umeme yenye urefu wa zaidi ya kilomita 617 ya msongo wa kilovolti 400 kutoka Iringa–Mbeya–Songwe, ambayo pia itaunganisha Mkoa wa Rukwa kwenye Gridi ya Taifa. Amesema pia ujenzi wa njia ya Songea–Tunduru–Masasi–Maumbika unaendelea kwa lengo la kuimarisha umeme katika Lindi na Mtwara, huku mkandarasi akiwa anaendelea na kazi Tunduru.

Amesema Serikali imeendelea kuwekeza katika Kituo cha Kupokea Umeme cha Ibadakuli mkoani Shinyanga, ambacho kitaboreshwa kutoka msongo wa kilovolti 220 hadi 400, hatua itakayoongeza uwezo wa kusafirisha umeme kutoka Dodoma kupitia Singida na Tabora hadi Shinyanga. Ameongeza kuwa hatua hiyo itaenda sambamba na kuanza kwa mradi wa Tanzania–Uganda Interconnector, ambao utasaidia kusafirisha umeme kuelekea Geita na Kanda ya Ziwa kwa ajili ya shughuli za madini na shughuli nyingine za kiuchumi.

Ndejembi amesema pamoja na kuongezeka kwa uzalishaji wa umeme, Serikali bado ina kazi ya kuboresha miundombinu ya usafirishaji na usambazaji, hasa katika maeneo ambayo umeme umekuwa ukikatika kutokana na uchakavu wa miundombinu. Amesema Serikali imejizatiti kuwekeza katika maboresho hayo ili ziada ya umeme inayozalishwa iweze kuwafikia wananchi kwa uhakika na kupunguza changamoto za kukatika kwa umeme.

Amesema mahitaji ya umeme nchini yanaendelea kukua kutokana na shughuli za kiuchumi na kijamii, hivyo Wizara itaendelea kutekeleza maelekezo na maono ya Rais Samia katika utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, ikiwemo lengo la kufikisha uzalishaji wa umeme hadi megawati 8,000 ifikapo mwaka 2030 kupitia vyanzo mbalimbali kama maji, gesi asilia, jua, upepo, makaa ya mawe na vyanzo vingine.

Ameeleza kuwa juhudi hizo zinaendelea katika maeneo mbalimbali, ikiwemo Kishapu mkoani Shinyanga ambako tayari kuna mradi wa megawati 50, huku Serikali ikiwa imesaini mkataba wa kuanza mradi wa umeme wa jua wa megawati 100. Aidha, Serikali inalenga kuzalisha angalau megawati 130 kupitia nishati ya jotoardhi, hatua ambazo kwa pamoja zinalenga kujenga mfumo wa nishati wenye uzalishaji mkubwa, usafirishaji imara na usambazaji wa umeme wa uhakika kwa maendeleo ya Tanzania.

Post a Comment

Previous Post Next Post