Ndoto imetimia na mpango wa kuwa na umeme wa uhakika umewezekana-Rais Samia



Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, amesema kukamilika kwa Mradi wa Bwawa la Kuzalisha Umeme la Julius Nyerere ni utekelezaji wa ndoto ya muda mrefu ya Tanzania ya kuwa na umeme wa uhakika kwa ajili ya kuchochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii.

Rais Samia amesema Serikali ilitekeleza mradi huo kwa uzito unaostahili kutokana na umuhimu wake mkubwa kwa maendeleo ya Taifa, akieleza kuwa hakukuwa na namna ya kuuacha mradi huo kutokana na mchango wake unaotarajiwa katika kuimarisha upatikanaji wa umeme nchini.


Akizungumza leo Jumamosi, Agosti 22, 2026, wakati akizindua rasmi mradi huo Mkoani Pwani, Rais Samia amesema ni jambo la furaha kushuhudia kukamilika kwa mradi ambao kwa miaka mingi umekuwa sehemu ya mipango na jitihada za Serikali za kuhakikisha Tanzania inakuwa na umeme wa uhakika.

Rais Samia amekumbusha kuwa Desemba 22, 2022 alifika kushuhudia hatua ya kufungwa kwa njia ya kuchepusha maji ya Mto Rufiji na kuanza kujazwa kwa maji katika bwawa hilo, akisema awali ilitarajiwa bwawa hilo kujazwa ndani ya kipindi cha miaka mitatu, lakini kwa neema ya Mungu lilijaa ndani ya mwaka mmoja na nusu na kuwezesha kuanza kwa majaribio ya uzalishaji wa umeme.

Katika uzinduzi huo, Rais Samia amezindua kituo cha kuzalisha umeme, kutembelea mitambo ya kuzalisha umeme, tuta kuu pamoja na kituo cha kupokea na kusafirisha umeme kwenda kwenye Gridi ya Taifa, akisema maeneo yote yanafanya kazi na hilo ni jambo la fahari kwa Tanzania.

Mradi wa Bwawa la Julius Nyerere una uwezo wa kuzalisha Megawati 2,115 za umeme, hatua inayotarajiwa kuongeza kwa kiasi kikubwa uwezo wa Tanzania kuzalisha umeme na kuwezesha upatikanaji wa nishati ya uhakika kwa shughuli za uzalishaji, uwekezaji na maendeleo ya wananchi. Rais Samia amesema kukamilika kwa mradi huo kunathibitisha kuwa ndoto iliyowekwa na Serikali imefanikiwa na mpango uliowekwa umewezekana.

Post a Comment

Previous Post Next Post