Na Mwandishi Wetu
WANAFUNZI 85 wanatarajia kwenda masomoni kwenye vyuo vikuu mbalimbali nchini India kuanzia wiki ijayo kupitia Wakala wa Elimu Nje ya Nchi Global Education Link (GEL).
Wanafunzi hao na wazazi wao walihudhuria mkutano uliofanyika katika ofisi za GEL mwishoni mwa wiki kwaajili ya kupewa mafunzo ya namna ya kuishi nchini humo.
Pia walielezwa mambo wanayotakiwa kufanya na wasiyotakiwa kuyafanya wakiwa masomoni nchini humo ikiwemo suala la vibali, bima na makaazi ili waweze kuhitimu masomo yao.
Mbali na mafunzo hayo walipewa tiketi zao za ndege, visa na nyaraka mbalimbali zitakazowawezesha kupokelewa kwenye vyuo wanavyokwenda kusoma nchini India.
Wanafunzi hao wanatarajiwa kuanza kwenda nchini India kuanzia tarehe 21 na 23 mwezi huu.
Akizungumza kwenye mkutano huo wa wanafunzi na wazazi wao, Mkurugenzi Mkuu wa GEL, Abdulmalik Mollel aliwataka wanafunzi hao kusoma huku wakiangalia fursa mbalimbali ambazo zinaweza kuwasaidia wanapohitimu.
“Tunahitaji GPA nzuri lakini pia huko kuna fursa nyingi sana, mtasoma na watoto wa matajiri wenye viwanda tunataka muwe karibu na watu kama hao kutambua fursa ya wewe kupata kazi siyo unamaliza halafu unakuja kuhangaika kutafuta kazi wakati huko kulikuwa na fursa,” alisema
Aliwataka wanafunzi hao kutafuta marafiki ambao wataongeza thamani ya masomo yao badala ya kuwa na marafiki ambao wanapenda starehe na hawahudhuriii masomo madarasani.
“Katumieni muda wenu nje ya kile kilichowapeleka kwa maana ya kujiongeza, tatizo la ajira ni shida ya dunia nzima siyo Tanzania ni wewe tu unavyoona fursa unazoona hata kwa wanafunzi utakaosoma nao huko nje,” alisema
“Kule mtakutana na wanafunzi wa mataifa mbalimbali na hata wa nchi zilizoendelea ulizeni fursa zilizoko kule kwenye mataifa yao ili kama ukimaliza unaweza kwenda kufanya kazi siyo lazima uje kuhangaika baada ya kuhitimu,”
“Mfano mtasoma na watoto wa matajiri wana viwanda ulizeni fursa zilizoko kwa hao watoto kwasababu India watu kuwa viwanda vidogo vidogo nyumbani kwao ni maisha ya kawaida kabisa kuna mtu ana kiwanda chumbani kwake thamani ya mtaji ukiuliza ni Dola 8,000,” alisema
Alisema India kuna viwanda vidogo vidogo ambavyo mtaji wake ni mdogo kiasi kwamba hata ndugu wanaweza kukupa na aliwataka kuondokana na dhana kwamba kuanzisha biashara kunahitaji mabilioni ya fedha.
“India wameendelea sana kwa viwanda tumieni fursa hiyo ila isikutoe kwenye reli ya nasomo yako. Jiulize unasoma kwaajili ya GPA nzuri tu au unakwenda kuhamisha maarifa ya kuchukua telnolojia na fursa za viwanda zinazopatikana kule kuleta hapa Tznania,” alisema Mollel
Alisema kila mwaka wanafunzi zaidi ya 800 wanapitia Global Education Link kwenda kusoma nje ya nchi hivyo kila mmoja akiwa mbunifu na kubaini fursa zilizoko nje ya nchi watapunguza tatizo la ajira wanapohitimu.
Alisema kuanzia mwakani Global Education Link itafungua fursa za ajira kwasababu kuna kampuni kubwa nchini ambazo zimekuwa iwape wataalamu wa aina mbalimbali inaowafahamu.
Alisema India inaongoza kwa kupeleka vijana wao kwenda kufanya kazi nje na si kwa bahati mbaya bali ni kutokana na kuwa na mtandao wa kubaini fursa mbalimbali kwenye mataifa.
“Kule India hawasomi ili wapate GPA wanasoma ili watengeneze fursa wewe unasoma ukimaliza unaanza kulalamika hakuna ajira, hatutaki hilo.Tunatamani mpate zaidi ya GPA mrudi na fursa zinazopatikana huko,” alisema Mollel
“ Ulaya kuna shida kubwa ya rasilimali watu kutokana na wengi kustaafu kwa umri sasa wewe ukisoma uhandisi jiongeze soma na kijerumani au Kifaransa angalia lugha ambayo inaweza kukusaidia kupata ajira,” alisema
Alsiema kwenye mataifa ya Ulaya fursa za kazi zipo ila wanataka mtu anayejua lugha yao kwa hiyo aliwataka wanafunzi hao kuhakikisha wanapata fursa zote wanazoona huko wasiishie kukariri GPA.
from MALUNDE 1 BLOG https://ift.tt/TA7p4jm
Tags
News







