Aagiza afike Dodoma Januari 21, akikaidi atafuatwa kwa pingu
Halima Mdee naye aunganishwa katika shutuma, atakiwa Januari 22.
NA DOTTO KWILASA, DODOMA
SPIKA wa Bunge, Job Ndugai amemtaka Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Profesa Mussa Assad, kufika mbele ya Kamati ya Bunge, Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge, Januari 21 mwaka huu, kujibu tuhuma alizozitoa dhidi ya muhimili huo kuwa ni dhaifu.
Pia wito huo umemkumba Mbunge wa Kawe (Chadema) Halima Mdee, ambaye naye ametakiwa kuripoti mbele ya kamati hiyo, Januari 22 mwaka huu, kuthibitisha madai yake aliyoyatoa kupitia mitandao ya kijamiii kuwa Bunge ni dhaifu.
Spika Ndugai, amesema Bunge halina Polisi lakini linaweza kumleta mtu yeyote kwa pingu akiwemo Mkaguzi Mkuu huyo wa Hesabu za Serikali.
Desemba mwaka jana, akiwa nchini Marekani akihojiwa na Mwandishi wa Habari, Anord Kayanda, wa Idhaa ya Kiswahili ya Radio ya Umoja wa Mataifa (UN), Profesa Assad alieleza kuwa Bunge ni dhaifu.
Mtangazaji huyo alimuuliza CAG kuwa, ofisi yake imekuwa ikijitahidi kufanya ukaguzi na kutoa ripoti kila mwaka zenye kuonyesha ubadhilifu lakini bado wananchi hawaoni kinachoendelea.
Akijibu Prof. Assad alisema: “Kama tunatoa ripoti halafu hatua hazichukuliwi huo kwangu mimi ni udhaifu wa Bunge. Na Bunge linahitaji lisimamie kuhakikisha mahali kwenye matatizo hatua zinachukuliwa.
“Kazi yetu ni kutoa ripoti na huo udhaifu ni jambo la kusikitisha, lakini tunaamini muda si mrefu huenda likarekebishika. Lakini tatizo kubwa ni kwamba Bunge linashindwa kufanyakazi yake kama inavyotakiwa.”
Aidha, akizungumza jana Jijini hapa na waandishi wa Habari, Spika Ndugai alisema kama CAG anasema Bunge ni dhaifu basi mpotoshaji mkubwa atakuwa ni yeye na ofisi yake.
“Kwa hiyo sasa na kwa mujibu wa kinga madaraka na haki za Bunge kwa sheria za Tanzania. Na Kwa mujibu wa mamlaka niliyo nayo kama Spika, Kifungu cha 4, kifungu kidogo cha kwanza (a) cha nyongeza ya nane ya kanuni za kudumu za Bunge, Toleo la Januari mwaka 2016.
“Suala hili nalipeleka kwenye Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge, ili waweze kulifanyia kazi.
“Kwa hiyo CAG Profesa Assad, anapaswa kufika kwenye kamati Januri 21 mwaka huu, nakazia wito huu atokee tarehe 21 Januari na ajitokeze kwenye kamati na kuthibitisha maneno yake ya huko Marekani.
“Na mnafahamu pamoja na kuwa hatuna polisi, lakini tuna uwezo wa kumleta mtu kwa pingu, kwa hiyo natumaini wito huu, atauzingatia kwa sababu nataka kumhakikishia sisi si dhaifu,”alisema Spika Ndugai.
Katika hatua nyingine, Ndugai alimtaka Mbunge wa Kawe, Halima Mdee (Chadema) kufika mbele ya Kamati hiyo kujibu maneno aliyosema hivi karibuni kupitia mitandao ya kijamii akiunga mkono kauli ya Profesa Assad, kwamba Bunge ni dhaifu.
Mdee aliandika: Roho ya mwenendo wa nchi inategemea uimara wa Bunge, sasa CAG amesema Bunge ni dhaifu ni kweli mimi kama mbunge wa vipindi vitatu nathibitisha hilo.
Ndugai alisema: “Na mkumbuke Mdee tumeshampa adhabu kadhaa kwa kushindwa kutawala mdomo na ulimi wake, namuhakikishia hatujachoka na yeye atokee kwenye kamati apate haki yake ya kusikilizwa.”
Alisisitiza kuwa, ikiwa CAG anatoa kauli hiyo imelenga kutoa picha kwamba ripoti zake hazifanyiwi kazi au akishazifikisha bungeni kazi inakuwa imekwisha, jambo ambalo si kweli.
“CAG na maofisa wake wanaingia kwenye Kamati ya Kudumu ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) pamoja na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mashirika ya Umma (PAC),” alisema Ndugai.
Spika alisema kuwa ripoti hizo zikifika kwenye kamati hizo ambazo zinaongozwa na upinzani, muda wote maofisa wa CAG wanakuwepo kueleza mapungufu waliyoyabaini na hatua zinazopaswa kuchukuliwa.
Alisema, tangu Serikali ya Awamu ya Tano ilipoingia madarakani, imekuwa ikipambana dhidi ya matumizi mbaya ya fedha za umma na hatua zimekuwa zikichukuliwa.
Spika ambaye pia ni Mbunge wa Kongwa (CCM), alisema mabadiliko makubwa kwenye usimamizi wa fedha za umma yamefanyika kwa ushauri wa Bunge na CAG, hivyo alishangazwa na hatua zipi ambazo CAG alitaka zichukuliwe.
from Jamvi La Habari http://bit.ly/2QAMoK4
