Mafunzo ya uendeshaji wa mradi awamu ya pili yaanza kutolewa kwa vijana wa kitanzania
Zipo awamu 11 za mafunzo katika sekta zote za reli na huduma.
NA JONAS MUSHI
MRADI wa ujenzi wa reli ya kisasa SGR awamu ya kwanza kipande cha Dar es Salaam hadi Morogoro kimefikia asilimia 42 huku kazi kubwa ikiwa ni kuweka mataluma kwenye tuta, kulaza reli na ujenzi wa madaraja.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, baada ya kufungua awamu ya pili ya mafunzo ya uendeshaji na usimamizi wa reli kwa wataalamu na wahandisi, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania (TRC), Mhandisi Masanja Kadogosa, alisema kipande hicho kinatakiwa hadi Novemba mwaka huu kiwe kimekamilika ili kianze kufanya kazi.
Alisema, kwa mujibu wa tathmini iliyofanyika kipande hicho chenye umbali wa kilomita 300 kitahitaji wafanyakazi 167 katika uendeshaji na kukisimamia.
Kutokana na mahitaji hayo alisema, TRC imeanzisha mafunzo kwa wahandisi na wataalamu mbalimbali wa shirika hilo ikiwa ni maandalizi ya kuwa na waendeshaji na wasimamizi wa mradi huo ambao ni mara ya kwanza kuwa nao hapa nchini.
“Tuna awamu 11 za mafunzo ambapo Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano alitufungulia mafunzo haya na tukaanza na kumaliza awamu ya kwanza ambapo jumla ya wataalam 33 walipatiwa mafunzo na leo (jana) tumeanza awamu ya pili ambayo inajumuisha wataalamu 22 watakaopata mafunzo ya uendeshaji na usimamizi wa reli,” alisema Kadogosa.
Naye Kaimu Mkurugenzi wa Miundombinu ya Reli, Mhandisi Felex Nlalio, aliwasisitiza walaatamu hao kuwatumia walimu wa mafunzo hayo kupata ujuzi wa hali ya juu kwa kuuliza maswali na kujisomea.
“Hawa walimu muwatumie vizuri kwa kuuliza maswali yakutosha pale ambapo hujaelewa kitu chochote kwasababu wakishaondoka huwezi tena kuuliza kitu labda ufanye kwa barua pepe ambayo anaweza akujibu au asikujibu,” alisema Nlalio.
Kwa upande wake Meneja wa ujenzi wa kipande cha Dar es Salaam hadi Morogoro, Mhandisi Machibya Masanja, alisema tayari reli zimeshalazwa kipande cha kilometa 30 na wameshanza kusimika nguzo za umeme huku wakiendelea kukamilisha madaraja.
Reli ya Kati ya kiwango cha kimataifa (standard gauge) ambayo ujenzi wake unaendelea, inatarajiwa kujengewa njia ya juu (flyover) yenye urefu wa kilomita tano kuanzia Bandari ya Dar es Salaam hadi Ilala.
Reli inayojengwa itakuwa na uwezo wa kupitisha treni itakayokuwa na uwezo wa kubeba kati ya tani 30 hadi 35 kwa ‘excel’ moja na kwa mwaka itaweza kusafirisha tani milioni 17 za mizigo.
Uzito huu ni zaidi ya mara tatu ya uzito wa mizigo inayosafirishwa na treni inayotumika sasa ambayo husafirisha tani milioni 5 tu kwa mwaka.
Isitoshe treni hiyo itakuwa na uwezo wa kubeba tani 10,000 za mizigo kwa mara moja, uzito ambao ni sawa na ule wa mizigo inayoweza kubebwa na malori ya ‘semi trailer’ 500.
Pia itakuwa na kasi ya kilometa 160 kwa saa kwa treni ya abiria na kasi ya kilometa 130 kwa saa kwa treni ya mizigo ambapo inakadiriwa kutumia saa tatu kutoka Dar es Salaam hadi Dodoma.
Reli hiyo inatarajiwa kuimarisha biashara ya ndani ya Bara la Afrika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati ambazo zimekuwa zikitumia bandari ya Dar es Salaam kupitishia mizigo kutoka nje ya Afrika. Sasa hata mtu anayeishi Dodoma atakuwa na uwezo wa kufanya kazi Dar es Salaam.
Kiuchumi Tanzania ina bandari sawa na Kenya ambayo kwa faida kiuchumi inaweza kuchukuliwa kama faida linganifu (comparative advantage), lakini haitoshi na haitakuwa na faida kama hakuna miundombinu itakayoifanya kushindana na nchi nyingine.
Ili bandari iwe na faida ni lazima kuwa na miundombinu mizuri ili kutoka kuwa ‘comparative advantage’ na kuwa ‘competitive advantage’ (faida shindani) itakayoweza kushindana na nchi nyingine zenye bandari kama Tanzania.
from Jamvi La Habari http://bit.ly/2H3FYDA
