Na Mwandishi Wetu
SERIKALI inatarajia kutumia Sh Tirioni 1.3 kupitia mkopo kutoka Exim Bank ya India, kwa ajili ya miradi ya maji katika Miji 28 nchi nzima, ili kukabiliana na tatizo la maji.
Hayo yamebainishwa jana na Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Profesa Kitila Mkumbo
alipofanya ziara katika Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira Jijini Tanga (Tanga-Uwasa) na kuzungumza n watumishi wa mamlaka hiyo.
Profesa Mkumbo, alifanya ziara katika mamlaka hiyo kwa ajili ya kujionea utendaji wa kazi na zaidi kuona changamoto zinazowakabili watumishi hao na mamlaka husika na namna ya kuzitafutia ufumbuzi.
Alisema, katika fedha hizo zaidi ya Sh Bil 140 zitainufaisha Miji ya Pangani, Muheza na Korogwe, ambapo matarajio ya Serikali ni kuhakikisha kufikia malengo ya kufikisha maji kwa asilimia 85 vijijini na 95 mijini hadi kufikia mwaka 2025.
Aidha, alisisitiza kuwa katika Miji hiyo Pangani imetengewa kiasi cha Sh Bil 22.5, Muheza Bil 5.6 na Korogwe kupitia mradi mkuu wa maji Korogwe na Handeni zimetengwa Bil 112.5.
“Hizi fedha tutahakikisha tunafuatilia kila hatua ya utekelezaji wake, hatutaki kurudia makosa na kuishia kubaki na mabomba matupu huku maji hayatoki, malengo tuliyojiwekea hadi kufikia 2025 tunataka yatimie si mameno matupu,” alisema Profesa Mkumbo.
Aidha, alisema mchakato wa miradi hiyo umekwishaanza kwa hatua za awali ya usanifu na kupata mtaalamu mshauri kwa ajili ya miradi hiyo, katika Miji ambayo
imebainishwa kunufaika nchi nzima.
“Hadi kufikia Juni mwaka huu, miradi hii itakuwa imekwishasainiwa na Septemba wakandarasi watatakiwa kuwa katika maeneo ya kazi katika miji hiyo 28, kwa ajili ya kutekeleza miradi,” alisema.
Hata hivyo, alitumia fursa hiyo kuwataka makandarasi kuhakikisha wanafanyakazi kwa uwadilifu na watambue Serikali haitomdhulumu yeyote na fedha zao zitalipwa bila ya mashaka wala kuchelewa.
“Tunajua madai ya makandarasi wengi nchi nzima, lakini tutawalipa waondoe shaka kila mwezi tutalipa Sh bil 8 hadi 12, hivyo tutawalipa tu,” alisema.
Awali akizungumza katika kikao hicho, Mkurugenzi wa Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Jijini Tanga (Tanga-Uwasa) Mhandisi Geofrey Hilly alisema, changamoto kubwa kwa sasa mkoani hapo ni namna ya kuongeza huduma ya maji taka ndani ya Jiji.
“Mbali na fedha zilizoainishwa na Katibu Mkuu, lakini tunataraji kupokea zaidi ya Sh bil 400 kwa ajili ya miradi ya maji taka, kubadilisha miundombinu ya mabomba, ujenzi wa matanki na miundombinu mingine,” alisema Mhandisi Hilly.
from Jamvi La Habari http://bit.ly/2SJ2H9x
