Wahadhiri wa Vyuo wausifu muswada vyama vya siasa

NA JONAS MUSHI

WAKATI baadhi ya vyama vya siasa vikiupinga Mswada wa Sheria ya Vyama vya Siasa, Wahadhiri wa vyuo vikuu nchini wameibuka na kuelezea faida za muswada huo huku wakitoa wito wa vyama vya siasa kupewa elimu zaidi kuhusu dhana ya demokrasia.

Akizungumza na JAMVI LA HABARI kwa njia ya simu kupata maoni yake kuhusu muswada na malalamiko ya baadhi ya vyama vya upinzani, Mhahiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk. Benson Bana, alisema anashangazwa kuona wanasiasa wakilalamikia muswada ambao umetokana na maoni yao na wadau wote wa siasa ikiwemo taasisi aliyopo yeye(UDSM).

“Muswada huu haujatoka hewani tulitoa maoni wakiwemo hao wanaolalamika na taasisi niliyopo pia tulipewa fursa hiyo, wengine wakachangia kwa maandishi wengine kwa mikutano na majadiliano na mwisho ukapatikana huu muswada,” alisema Dk. Bana.

Alisema ni jambo la kusahangaza kuopna wanasiasa wanakwenda kuupinga mahakamani ukiwa bado haujajadiliwa bungeni na kupitishwa kuwa sheria.

“Wabunge wetu si ma-mbumbu wale ni wawakilishi wa wananchi wana akili wataenda kukaa na kuuchambua, kuujadili na kuupigia kura na kama ukipita na mtu hajaridhika ndiyo aende mahakamani kupinga hiyo sheria,” aliongeza.

Alisema hata kama muswada huo utakua sheria, upo utaratibu wa kufanya marejeo sheria za zamani na kurekebisha vifungu ambavyo vitaonekana havina tija kwa jamii husika hivyo, “hakukua na haja ya kuupinga muswada ambao haujui kama utakuwa sheria au la.”

Alisem ani vyema jamii iondokane na dhana ya kuwa muswada wowote ukifika bungeni utapitishwa kwasababu ya kuwepo wabunge wengi wa CCM na kwamba hawawezi kupitisha kitu ambacho ni kibaya kwa jamii ambayo na wao miongoni mwa wanajamii hao.

Akizungumzia malalamiko ya baadhi ya vyama kwamba wanakwenda kuingiliwa na msajili katika mambo yao ya ndani, Dk. Bana alisema, “Duniani kote hakuna demokrasia isiyo na mipaka na mtu anapovuka mipaka ile lazima hatua zichukuliwe, na kama msajili amekupa usajili na kukupa mipaka ukishindwa kuifuta ndiye mwenye mamlaka ya kuwajibisha.”

Alisema haiwezekani vyama viwepo pasipo taasisi ya udhibiti ambayo itavisimamia vyama hivyo katika shughuli zake na kuhakikisha vinafuata sheria zilizowekwa.

Dk. Bana ambaye ni mhadhirio katika kitivo cha sayansi za jamii na sanaa alisema anaona kuna uhitaji wa elimu zaidi kutolewa kwa wanasiasa kuhusu dhana ya demokrasia kwani inaonekana wengi wao hawaelewi.

“Dhana ya demokrasia haimaanishi kuwa ukishasajili chama basi wewe uachiwe kufanya unavyotaka na uwe juu ya kila kitu kwasababu ndiyo mwenyekiti wa chama basi unaamua lolote. Hapana. Lazima kuwepo mamlaka rekebu.” alisema Dk. Bana.

Naye Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Ruaha,(RUCO) Dady Igogo, alisema hofu kubwa ya wanasiasa wa upinzani ni kuona kuwa sheria hii inakwenda kuvifuta “vyama vya kwenye mikoba” ambavyo huwa havifuati sheria.

“Muswada huu ukipitishw ana kuwa sheria unakwenda kusimamia matumizi ya ruzuku, kuondoa umungu mtu kwenye vyama, hivyo hauwezi kukubalika na vyama vya wapiga dili ndiyo maana wanapinga,” alisema Igogo ambaye amewahi pia kuwa Naibu Meya wa Manispaa ya Iringa kupitia Chadema.

Alisema muswada huo ukipitishwa utakwendakujenga uwajibikaji, utawala bora na matumizi mazuri ya fedha ndani ya vyama na kufutilia mbali vyama vitakavyoshindwa kufuata misingi na mifumo hiyo.

Jana gazeti hili, lilitoa taarifa kuhusiana na kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa asasi ya kiraia inayojihusisha na masuala ya maendeleo ya jamii ya Alliance for Development Organisation (ADOR), Habibu Mchange, kusema  Muswada wa Sheria ya Vyama vya Siasa unajibu malalamiko ya muda mrefu ya wanachama wa vyama vya upinzani kwa kuondoa ukiritimba wa mtu mmoja kumiliki chama.

Mchange ambaye amefanya siasa za upinzani kwa muda mrefu alisema mswada huo una mabadiliko mazuri yaliyolenga kuvifanya vyama kuwa taasisi zinazofuata sheria kikamilifu.

Alisema kutokana na mabadiliko hayo yenye tija kwa vyama vya siasa na Taifa yatakwenda kuwabana viongozi wa vyama waliozoea kuviendesha pasipo kufuata sheria wameamua kukimbilia mahakamani kupinga usijadiliwe bungeni.

Mchange ambaye amekuwa mwananchama na Chadema na ACT Wazalendo kwa nyakati tofauti na kufanikiwa kushika nyadhifa mbalimbali ndani ya vyama hivyo, alisema migogoro mingi inayoibuka ndani ya vyama hivyo mara kwa mara inatokana na kukosekana kwa chombo chenye mamlaka ya udhibiti wa vyama vya siasa.

“Muswada huu ndiyo suluhu ya migogoro inayotokana na mtu mmoja ndani ya chama kukataa kuachia madaraka na sasa inakwenda kuweka ukomo wa muda wa mtu kuwania uongozi ndani ya chama ili kuwapa nafasi wanachama wengine kukua kisiasa,” alisema Mchange.

Alitolea mfano wa mgogoro uliowahi kutokea mwaka 2008, 2009 na 2013 ndani ya Chadema baada ya baadhi ya wanachama wake kuonesha nia ya kutaka kugombea nafasi ya Uenyekiti kwa kufuata taratibu.

Aliwataja marehemu Chacha Wangwe, Zitto Kabwe, Profesa Kitila Mkumbo na Mwigamba kuwa ni miongoni mwa majeruhi wa kutokuwepo kwa sheria ya udhibiti wa vyama vya siasa na kuishia kufukuzwa kwenye vyama vyao kwa kutaka nafasi ya uenyekiti kwa mujibu wa sheria.

“Kwa sheria tuliyonayo mtu ukiwa na mgogoro ndani ya chama ukienda kushtaki basi jua wewe si mwanachama tena lakini kwa sheria hii inayokuja mwanachama anapewa sehemu ya kukata rufaa na kupewa haki yake ndani ya chama,” alisema na kuongeza, “tumewahi kukandamizwa kwa kukosekana hii sheria. Mwigamba aliwahikupigwa makofi kweye mkutano Arusha lakini hakuwa na pa kwenda kulalamika.”

Alisema imekuwa ni jambo la kawaida kwa viongozi wakuu wa vyama kuwatisha wanaotaka nafasi zao na hivyo kuwafanya kuendelea kubakia madarakani tena bila kupingwa wakati wa chaguzi.

“Wanalilia demokrasia lakini ndani ya vyama vyao hakujawahi kuwa na wagombea wa kuwania nafasi za juu wamekuwa wao tu tangu miaka ya tisini hadi sasa Freeman Mbowe ni Mwenyekiti wa Chadema, Ibrahim Lipumba ni mwenyekiti wa CUF, Maalim Seif ni Katibu Mkuu wa CUF wanataka watawale hadi wafe,” alisema

Alisema sheria ya sasa atakwenda kuondoa “umungu mtu” na mtu mmoja kumiliki chama akitolea mfano kitendo cha Mbowe kuwahi kufuta uteuzi halali wa wabunge wa viti maalum mwaka 2010 na kupanga upya alivyotaka yeye.

Alitaja udhibiti wa matumizi ya fedha za chama kuwa ni sehemu ya sheria mpya inayokuja kwa lengo la kudhibiti na kusimamia matumizi ya fedha za zuruku ambazo ni kodi za wananchi tofauti na ilivyo sasa.

Alisema uzuri wa sheria hiyo tofauti na ya sasa inatoa adhabu mbadala kabla ya adhabu ya kukifuta chama kwa kushindwa kufuata sheria.

“Kwa sheria ya sasa chama kikikiuka sheria adhabu iliyowekwa ni moja tu ya kufutwa mfano ACT-Wazalendo na Chadema waliposhindwa kuwasilisha nyaraka za mahesabu yake walitakiwa wafutiwe usajili lakini sasa tunaenda kuwa na sehria inayosema kama chama kina matatizo ya fedha ama kitapata hati chafu,” alisema na kuongeza kuwa anaunga mkono muswada huo kwasababu umetii kiu yake ya kutaka fedha za wananchi zisimamiwe.

“Chama cha Mapinduzi (CCM) inapokea ruzuku ya milioni 900 kwa mwezi, Chadema milioni 360, CUF milioni 161 na ACT-Wazalendo milioni 4.2 na zukuku ni fedha za wananchi lakini ahakuna mamlaka ya kuzisimamia wanaamua wenyewe wazitumie vipi lakini sasa inapendekezwa sheria ambayo inatoa zuruku na inadhibiti matumizi yake lakini hawa jamaa hawataki,” alisema.

Alisema anaishukuru serikali kwa kuleta mswada huo wakati sahihi ambao yeye kama mwanasisa mchanga pamoja na wenzake wakiwa kwenye vyama vyao waliwahi kukandamizwa kwa kukosekana kwa sheria ya namna hiyo.

Aliongeza kuwa pamoja na wanasiasa wanaopinga mswada huo kuwa na haki ya kwenda mahakamani kikatiba lakini wangepaswa kuwa na hoja za msingi badala ya hoja za kuhisi.

“Hoja yao ni kwamba wanahisi mswada ule ukienda kujadiliwa na kupitishwa watanyimwa baadhi ya haki zao,” alisema na kuongeza, “itakuwa ni mahakama ya ajabu kuwahi kutokea kufanyia uamuzi na kutolea hukumu hoja za kuhisi.”

Alisema ni vyema wabunge kujitokeza kuujadili mswada huo kama wanavyotakiwa kisheria na baadae kuupigia kura na kwamba kidemokrasia wengi ndiyo watakaoshinda.

“Wanasiasa waliokwenda mahakamani kupinga mswada huu ambao unakwenda kusimamia fedha zetu walipa kodi zisitumike vibaya, usijadiliwe wanaitwa wanasiasa majuha na sisi tutawaambia watanzania ukweli na uzuri wa mswada huo,” alisema Mchange.

Aidha aliwahasa watanzania na wanasiasa nchini kusaidia kuijenga sheria hiyo ambayo itasaidia kuondoa uungu mtu ndani ya vyama, kukuza vipawa kwa kuachiana madaraka na kutokuwepo na umiliki wa vyama.



from Jamvi La Habari http://bit.ly/2QwJo14

Post a Comment

Previous Post Next Post