Kisarawe yatoa Hekari 200 kujenga Chuo cha VETA, DC Jokate azungumza
Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) imekabidhiwa na Halmashauri ya Wilaya ya Kisarawe, mkoani Pwani jumla ya Hekari 200 kwa ajili ya kusaidia kupanua shughuli za utoaji elimu na mafunzo ya ufundi stadi.
Akizungumza kabla ya makabidhiano ya eneo hilo, Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe Jokate Mwegelo alisema ni bahati kubwa kwa VETA kupata eneo hilo ambalo limekaa kimkakati kutokana na kuwa na miundombinu muhimu na kuzungukwa na maeneo muhimu kiuchumi..
“Mkoa wa Pwani tumejipambanua kama mkoa wa viwanda. Lakini ili viwanda viwanufaishe vyema wananchi wa Kisarawe kuna mahitaji makubwa kwa vijana kupata ujuzi kwa ajili ya kufanya kazi kwenye viwanda. Kwa hiyo tunaona ni jambo la msingi VETA waje watusaidie kuinua ujuzi kwa vijana wetu," amesema DC Jokate.
Vilevile, alisema eneo hilo liko jirani na ukanda maalum wa kiuchumi (special economic zone), ambao unaweza kutoa fursa kwa vijana kupata maeneo ya kufanyia mazoezi ya vitendo na ajira baada ya kuhitimu mafunzo yao..
Naye Mkurugenzi Mkuu wa VETA, Dkt. Pancras Bujulu aliushukuru uongozi wa Wilaya na Halmashauri ya Wilaya ya Kisarawe kwa kuwa tayari na kwa wepesi kutoa eneo hilo kwani litasaidia kwa kiasi kikubwa kupanua shughuli za mafunzo ya VETA, hususani kwa kanda ya Dar es Salaam.
No comments