Breaking News

Viongozi katika taasisi nne Muhimbili wakutana kuboresha huduma kwa Wagonjwa


Viongozi wa taasisi nne; Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Taasisi ya Mifupa Muhimbili (MOI), Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) na Hospitali ya Taifa Muhimbili-Mloganzila zimekutana  kujadiliana jinsi ya kuboresha huduma za matibabu kwa wagonjwa wanaotibiwa katika taasisi hizo.

Akizungumza na Viongozi hao, Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Prof. Lawrence Museru ambaye amekuwa Mwenyekiti wa mkutano huo, amewaomba wakurugenzi wenzake kuendelea kuimarisha ushirikiano na kuandaa mikutano ya mara kwa mara baina ya taasisi hizo.

Katika mkutano huo, wakurugenzi na wakuu wa idara wamekubaliana kuimarisha mawasiliano katika taasisi hizo ili kuhakikisha wagonjwa wanaendelea kuonwa na wataalam kwa wakati.

“Sisi kama wakurugenzi tuendelee kuwahimiza madaktari na watalaamu wengine kuimarisha mawasiliano yao na wagonjwa ili kuwapa fursa ya kujua mwendendo wa matibabu yao,” alisisitiza Prof. Museru.

Alisema uwepo wa mawasiliano mazuri baina ya watoa huduma na wananchi wanaohudumiwa utapunguza malalamiko yanayojitokeza mara kwa mara kuhusu mwenendo wa matibabu kwa wagonjwa.

Pia, katika mkutano huo, taasisi hizo zimekubaliana kutumia miundombinu iliyopo kwa ajili ya kuwahudumia wagonjwa endapo taasisi moja itakua imeelemewa.

“Kwa mfano, MOI au Muhimbili inaweza kulaza wagonjwa wa ICU wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete kwa muda kama ICU yao imejaa huku wakisubiri kupata nafasi ya kitanda katika taasisi hiyo ya Moyo,” amesema Mkurugenzi huyo.

Taasisi hizo zitakuwa zikikutana mara kwa mara ili kujadiliana changamoto mbalimbali zinazojitokeza, huku lengo kubwa likiwa ni kuboresha huduma za matibabu zinazotolewa MNH, MOI, JKCI na Muhimbili- Mloganzila.





from MUUNGWANA BLOG http://bit.ly/2SQmQxp

No comments