Breaking News

Kiwanda cha Mati chaanza kutengeneza Sanitizer kuwakinga wananchi dhidi ya Corona


Na John Walter, Manyara

Mkuu wa mkoa wa Manyara  Alexander Mnyeti  amewataka wakazi wa mkoa huo kuzingatia maelekezo yaliyotolewa na serikali na wataalamu wa afya ili kujikinga na maambukizi ya ugonjwa wa Corona unaoua na kuambukiza kwa kasi duniani.

Aidha amewaonya  wafanyabiashara wanaouza vitakasa mikono (Sanitizer) wenye tabia ya kubadilisha bidhaa husika  na kupoteza ubora uliopo na wanaouza bei ya juu tofauti na maelekezo ya serikali na kwamba  watakaobainika kufanya hivyo hatua Kali zitachukuliwa dhidi yao.

Amezungumza hayo wakati alipokitembelea kiwanda cha Mati super Brand Ltd Mjini Babati,ambacho licha ya kuwa kinatengeneza pombe kali kimeamua kushirikiana na serikali dhidi ya mapambano dhidi ya Corona  kwa kutengeneza Vitakasa mikono (Sanitizer) kwa ajili ya kusaidia watu kujikinga dhidi ya virusi vya Corona na kuziuza kwa bei elekezi ya serikali.

"Tujitahidi sana kujikinga,hicho ndo tunaweza,kwa sisi kwa nchi zetu hizi tukiruhusu ugonjwa uingie,usambae halafu ndo tutafute matibabu itatusumbua,kwa hiyo tujitahidi sana kwenye kujikinga kabla ugonjwa haujasambaa" alisisitiza Mnyeti

Ameupongeza uongozi wa kiwanda hicho kwa kujali afya za watu huku akiwataka waendelee kuzalisha kwa wingi bidhaa hizo ili wananchi wa mkoa huo waendelee kubaki salama.

Ameutaka uongozi wa Kiwanda hicho kuhakikisha bidhaa hiyo inasambazwa kwa wingi kwenye magulio,minada na masoko ili  wananchi wa kawaida waweze kuipata kwa haraka.

Yapo maeneo mtu hata kuoga hajawahi ana miezi Minne lakini akipata sanitizer akanawa, angalau itasaidia asisambaze haya matatizo' alisema Mnyeti.

Katibu tawala mkoa wa Manyara Missaile Musa ameeleza kuwa Bidhaa hiyo itasaidaia maeneo yenye shida ya maji,hivyo atawasiliana na walipo wilaya za pembezoni ili wazisambaze kwa wananchi kwa kuwa uhitaji ni mkubwa.

Mkuu wa wilaya ya Babati Elizabeth Kitundu ameupongeza uongozi wa Mati Super brand kwa uzalendo waliouonyesha.

David Mulokozi Mkurugenzi Mtendaji wa Mati Super Brand  Ltd amesema wameamua kutengeneza Sanitizer ili kuwasaidia wananchi waweze kujikinga dhidi ya virusi vya Covid 19 kwa kuwauzia kwa bei ya shilingi 1500 chupa ndogo, 2500 mili Lita 100,Lita tatu shillingi 75,000 na Lita 5 watauza kwa shiligi 12,500.

Mulokozi amechukizwa na baadhi ya wafanyabiashara waliotumia ugonjwa huo kama fursa ya kujipatia kipato kikubwa kwa kupandisha bei huku wengine wakichakachua na kuuza Sanitizer feki.

from MUUNGWANA BLOG https://ift.tt/2ymqYNg

No comments