Ilemela kinara urasimishaji na umilikisha makazi
Na James Timber, Mwanza
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela jijini Mwanza imeendelea kuongoza katika zoezi la urasimishaji na umilikishaji wa makazi holela nchini kwa kuandaa michoro ya mipango miji 58,000, kupima viwanja 52,000 na kumilikisha jumla ya viwanja 27,000.
Hayo yamebainishwa wakati wa zoezi la ugawaji wa hati miliki za viwanja 1508 kwa wananchi wa wilaya hiyo, Zoezi lililoendeshwa na Naibu Waziri wa wizara ya ardhi, nyumba na maendeleo ya makazi Mhe Dkt Angeline Mabula katika viwanja vya manispaa ya Ilemela ambapo amesema kuwa anaridhishwa na kasi ya upimaji na umilikishaji wa ardhi inayofanywa na wataalam wilayani humo sanjari na kuwaasa wananchi hao kumshukuru na kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Dkt John Magufuli kwa kuridhia kufanyika kwa zoezi la urasimishaji wa makazi holela
"Pamoja na changamoto zote mlizonazo, Ilemela kitaifa inaongoza katika zoezi zima la kupanga, kupima, na kumilikisha katika yale maeneo ya urasimishaji , Hongereni sana hata Mhe Waziri amekuwa akiwapongeza mara kwa mara," alisema
Aidha Mhe Dkt Mabula amezikumbusha kampuni zote za upimaji zinazoendesha zoezi la urasimishaji wa makazi nchini kutekeleza agizo lililotolewa na Waziri wa ardhi Mhe William Lukuvi la kukamilisha kazi zote zilizobaki ili kwenda sambamba na kasi ya Serikali ya awamu ya tano na kuwaondolea adha wananchi wanaohitaji huduma hiyo.
Kwa upande wake afisa mipango miji mkoa wa Mwanza Bwana Deogratias Kalemenze amesema kuwa kipindi cha miaka ya 1990 ilikuwa mtu yeyote anaejenga bila kufuata sheria na taratibu alilazimika kubomoa na kujenga upya tofauti na ilivyo sasa ambapo analipia gharama kidogo na kumilikishwa hivyo kuwataka wananchi kuitumia fursa hiyo adhimu ya urasimishaji makazi kuepuka usumbufu unaoweza kujitokeza na kusaidia Serikali kukusanya kodi ya pango la ardhi ili kutekeleza shughuli za maendeleo.
Nae kaimu mkurugenzi ambae pia ni afisa ardhi na mipango miji wa manispaa ya Ilemela Ndugu Shukran Kyando ametaja changamoto zinazokabili zoezi la urasimishaji na umilikishaji wa ardhi ikiwemo kasi ndogo ya wananchi kulipia gharama za umilikishwaji sambamba na kutaja hatua zilizokwisha chukuliwa mpaka sasa ikiwemo kutoa ilani ya siku 30 ya kuwataka wananchi hao kuja kumilikishwa ardhi hiyo.
Akihitimisha moja wa wananchi waliokabidhiwa hati miliki na naibu waziri wa ardhi Dkt Mabula, Bi Veronica Byengo kutoka mtaa wa Ghana amemshukuru Mhe Rais na Serikali ya awamu ya tano kwa kuendesha zoezi la urasimishaji huku akiwaomba wananchi wenzake kujitokeza kumilikishwa ardhi yao ili kujiepusha na migogoro isiyokuwa ya lazima na kuweza kukopesheka kwenye taasisi za kifedha.
from MUUNGWANA BLOG https://ift.tt/2V9fggN
No comments