Breaking News

Watu wanaohatarisha maisha kuwahudumia wagonjwa wa COVID -19



Kukiwa na watu milioni nne waliothibitishwa kuwa na maambukizi ya virusi vya corona, virusi hivi vimefanya mchango wa wauguzi kumulikwa.

Huwaogesha na kuwasafisha wagonjwa. Huwalisha wagonjwa wao na kufuatilia viashiria muhimu. Pamoja na majukumu hayo, uuguzi bado ni kazi yenye malipo madogo sana huku mchango wa wauguzi ukiwa hautambuliki katika sehemu nyingi duniani.

Katika kuadhimisha siku ya kimataifa ya wauguzi, BBC imezungumza na wauguzi wanne wanaofanya kazi katika mabara manne tofauti, ili kufahamu changamoto wanazokutana nazo katika mapambano dhidi ya virusi vya Covid-19.

Siku ya wauguzi husherehekewa tarehe 12 mwezi Mei, siku ya kumbukumbu ya kuzaliwa ya Florence Nightngale, mwana takwimu na mwanzilishi wa uuguzi wa kisasa

''Virusi vilikuwa na kasi. Hatukua na muda wa kujiandaa na kupanga,'' anasema muuguzi raia wa Uhispania Maria Moreno Jiménez.


Moreno Jimenez, 32 anafanya kazi katika hospitali kitengo cha ICU mjini Barcelona. Baada ya virusi vya corona kusambaa katika mji anaoishi mnamo mwezi Machi.

Maria na timu yake walianza mafunzo ya saa mbili kuhusu jinsi ya kutumia vifaa vya kujikinga .

''Mgonjwa wa kwanza kumshuhudia ilikuwa katikati ya mwezi Machi. Alikuwa na miaka ya 70 ,'' aliiambia BBC.

Mwezi mmoja wa uangalizi uliokoa maisha yake.

''Nilipomuona wodini, nilifurahi sana. Nilimwambia kuwa mimi ndiye niliyekuwa nikimuangalia alipokuwa kwenye chumba cha wagonjwa mahututi (ICU).''

Mgonjwa hakumuelewa vizuri Maria. Wagonjwa wengi hupatiwa dawa za kuwalaza usingizi wakiwa ICU na wale wanaokaa muda mrefu ndani ya vyumba vya wagonjwa mahututi wakati mwingine wanaweza kuwa katika hali ya kuchanganyikiwa.

''Si kama kwenye sinema, wagonjwa wanashukuru. Wagonjwa hawawi sawa na vile walivyokuwa awali walipofikishwa hospitalini kulazwa, hawakumbuki vitu vingi pia hawazungumzi sana.''

''Nilifurahi sana nilipojua kuwa anakwenda nyumbani.''

Mume wa Maria pia ni muuguzi katika hospitali hiyo hiyo. Baadhi ya wafanyakazi wenzao walipata maambukizi, ingawa kwa bahati nzuri hakuna aliyepoteza maisha na wengine wanaendelea kupata nafuu.


Baada ya Uhispania kuweka marufuku ya kutoka nje, watu walijenga kawaida ya kutoka nje kwenye vibaraza vyao na kuwashangilia kwa makofi wahudumu wa afya.

''Nchini Uhispania kuna kawaida ya kuwashukuru madaktari lakini huwasahau wauguzi.''

Moreno Jimenez ana matumaini kuwa hali hii itabadilika baada ya janga la corona kuisha.

''Wale pekee wanaolazwa ndio huelewa kazi yetu. Sasa kila mtu anajua tunachokifanya.''

''Ingekuwa vizuri sana kama watu wangetambuka kazi yetu. Ninafikiri moja kati ya vitu ambavyo watu wanaweza kufanya ni kututambua na kututaja.''

Gabriela Serrano, muuguzi anayefanya kazi nchini Marekani, ana kumbukumbu nzuri ya siku alipomuaona mgonjwa wake wa kwanza wa Covid-19 akiruhusiwa kurudi nyumbani.

''Alikuwa mwenye furaha sana, nilipokuwa nikimtoa nje ya jengo la hospitali. Alisema anahisi vizuri sana kuuona mwanga wa jua na kuvuta hewa safi ya nje''.


Serrano amekuwa muuguzi kwa miaka saba. Wakati wa janga alifanya kazi kwenye hospitali katika viunga vya mji wa San Francisco.

''Wagonjwa wawili wa Covid 19 niliokuwa nikiwahudumia walikuwa na maradhi mengine ya muda mrefu na walikuwa na umri wa zaidi ya miaka 70. Lakini walipoma. Hili linanipa matumaini.''

Gabriela, 31 alishuhudia vifo vya watu watatu ambavyo havikuwa kutokana corona miezi miwili iliyopita. Alieleza namna alivyoguswa na mwanamke aliyekua akielekea kuaga dunia.

''Alikuwa vizuri siku ya kwanza lakini alikuwa hazungumzi. Nilimueleza kila kitu nilichokuwa nikimfanyia, pamoja na kwamba hakuweza kunijibu.''

Siku iliyofuata , mgonjwa hakuwa akifumbua macho kabisa.

Hospitali ilitoa idhini mgonjwa atembelewe na nduguze katika saa zake za mwisho za uhai wake. Bahati mbaya, hakuwa na mtu wa karibu na rafiki yake mpenzi alichagua kukaa mbali na hospitali.

''Nilikaa naye, nikamshika mkono na kumwambia kuwa kila kitu kitakuwa sawa. kuwa niko naye , ajihisi ana mtu,'' alisema Gabriela.

''Sikujua kwa wakati ule kama alikuwa akinisikia, lakini lilikuwa jambo zuri kumfanyia.''




from MUUNGWANA BLOG https://ift.tt/2WOkkba

No comments