Afrika yaanza safari kuwafikishia umeme wananchi milioni 300
-Rais Samia ataka uunganishwaji
nguvu na wadau kuhakikisha mpango huo unafikiwa ifikapo 2030
-Wakuu wa Nchi wasaini
Azimio la Dar es Salaam lengo likiwa ni kuchochea maendeleo barani Afrika hususan
ya kiuhumi, nishati
Abraham Ntambara na Tunu Bashemela
Abraham Ntambaraa na Tunu Bashemela,
Dar es Salaam
WAKUU wa Nchi za
Afrika wamesaini kwa pamoja tamko la Azimio la Dar es Salaam ikiwa ni mkakati
wa utekelezaji wa kuwafikishia umeme wananchi milioni 300 barani Afrika.
Akizungumza kabla
ya kusaini azimio hilo wakati wa Mkutano wa Wakuu wa Nchi za Afrika kuhusu
Nishati ujulikanao kama “Missioni 300” mapema leo jijini Dar es Salaam Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan alisema nchi za Afrika
zinapaswa kuunganisha nguvu katika kuhakikisha wananchi wake wanafikiwa na
nishati ya umeme ili kuchochea ukuaji wa uchumi.
Rais Dkt. Samia alisema
Tanzania imepiga hatua kwa kusambaza umeme katika vijiji vyote na sasa inaweka
mkazo katika kufikisha nishati hiyo ngazi ya vitongoji.
“Mpaka sasa
tumefanikiwa kuunganisha umeme katika vijiji vyote 12,318 na vitongoji 32,827 kazi inayoendelea ni
kuunganisha umeme kwenye vitongoji 31,532 vilivyobakia kabla ya mwaka 2030,"
alisema Rais Dkt. Samia.
Rais Dkt. Samia alisema
kupitia mpango wa nishati Tanzania inafanya kazi ya kuongeza uzalishaji na
uimarishaji wa miundombinu ya usambazaji wa umeme akiongeza kuwa nchi za Afrika
lazima ziunganishe nguvu za wadau kwa lengo la kuwafikishia nishati ya umeme wananchi
milioni 300 kufikia 2030.
Aidha, alisema
Tanzania inatekeleza mkakati wa Taifa wa nishati safi ya kupikia wenye lengo la
kuwezesha wananchi wote kuondokana na madhara ya nishati ya kupikia isiyo safi
kutoka asilimia 10 za sasa hadi 80 ifikapo mwaka 2030.
Aidha, Rais Dkt. Samia
alisema Tanzania ni kitovu cha kuuza nishati ya umeme kwa nchi zinazoizunguka
zikiwemo Burundi, Rwanda, Kenya huku ikiendelea kuunganisha umeme kwa nchi za
Zambia na Uganda.
Awali akizungumza
wakati wa kumkaribisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuhutubia, Naibu
Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Dkt. Doto Biteko alisema Rais Dkt. Samia
amesimamia agenda ya nishati safi ya kupikia kwa kuhakikisha wananchi
wanafikiwa na nishati ya umeme.
Dkt. Biteko alisema Tanzania imeongeza uzalishaji wa umeme kutoka megawati 1,888 hadi 3,431. Mkutano huo wa Wakuu wa nchi za Afrika kuhusu nishati ulihitimishwa jana Januari,2025.
No comments